Windows

Yanga si riziki

Picha

YANGA jana imeng’oka kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam, FA, baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 katika mechi ya nusu fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.

Ushindi huo unaipeleka Lipuli fainali na sasa itacheza na Azam Juni 2, kwenye uwanja wa Ilulu, Lindi. Mshindi wa kombe hilo ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika. Kwa Yanga huo ni mchezo wa pili kupoteza katika uwanja huo kwani walipokutana kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara walifungwa bao 1-0 na wana Paruhengo.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga sasa kuomba Simba ifanye vibaya kwenye mechi zake ili itwae ubingwa jambo ambalo si la kulitarajia sana kwani Simba ina nafasi kubwa ya kutetea taji lake la Ligi Kuu.

Endapo itakosa ubingwa, Yanga itashuhudia tena mwaka mwingine ikiwa nje ya michuano ya kimataifa. Katika mechi ya jana iliyokuwa na kasi mwanzo mwisho huku kila timu ikitawala kwa kila kipindi, Lipuli waliandika bao la kuongoza katika dakika ya 27 kupitia kwa mshambuliaji Paul Nonga akimalizia mpira uliotemwa na mlinda mlango Clatous Kindoki wa Yanga baada ya piga nikupige kwenye langoni mwa wanajangwani hao.

Bao hilo lilionekana kuwapa nguvu wanapaluhengo hao ambapo waliendelea kutawala hasa sehemu ya kiungo katika pambano hilo na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara. Bao la pili la Lipuli liliwekwa kimiyani dakika ya 38 na Jimy Shoji aliyemalizia mpira uliotemwa kwa mara nyingine na Kindoki wakati wanawania mpira wa kichwa kwenye lango la Yanga.

Baada ya kuongoza kwa bao hilo la pili Yanga walianza kucharuka wakihaha kutengeneza mashambulizi kupitia winga zao lakini hata hivyo safu ya ulinzi ya Lipuli ilionekana kusimama imara kwa kuzima mashambulizi hayo yaliyokuwa yakiongozwa na Heritier Makambo. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikifanya mabadiliko ambayo hata hivyo hayakuzaa matunda na kipindi hiki Lipuli walicheza kwa kujilinda zaidi jambo lililowafanya washambuliaji wa Yanga kushindwa kuipenya ngome ya Lipuli.

Post a Comment

0 Comments