


MWANZA.WAKATI Biashara United ikishuka uwanjani kesho Ijumaa kuwakabili Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu,nyota wa kikosi hicho wameapa kufa na wapinzani hao kuhakikisha wanashinda na kujinasua nafasi za mkiani.
Yanga inawakabili Biashara United ikiwa na hasira za kupoteza mchezo wake muhimu wa kombe la Shirikisho dhidi ya Lipuli FC kwa kufungwa mabao 2-0 na kuondoshwa kwenye michuano hiyo hatua ya nusu fainali.
Pia mchzo huo ambao utapigwa kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma utakuwa mgumu,ikiwa Yanga wanataka kurudi kileleni,huku Biashara wakipambana kukaa nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Hadi sasa Yanga wapo nafasi ya pili kwa pointi 80 baada ya kucheza mechi 34,huku Biashara United wakiwa na alama zao 37 katika nafasi ya 18 baada ya kushuka uwanjani mara 33.
Nahodha wa timu hiyo Abdulmajid Mangalo alisema ili kujinasua nafasi za chini kwenye msimamo hawana budi kushinda mchezo wa leo dhidi ya Yanga na kujiweka nafasi nzuri.
Alisema kwa sasa mechi zilizobaki hawana masihara kwani nia yao ni kuhakikisha wanaibakiza timu kwenye Ligi Kuu msimu ujao,hivyo leo Yanga wasitarajie mteremko na kwamba wamejipanga vizuri.
“Tunawaheshimu sana Yanga kwa sababu ni timu kongwe,lakini kutokana na mahitaji yetu kwenye Ligi lazima tushinde,tutakuwa makini kusikiliza na kufuata maelekezo ya Kocha ili kufikia malengo yetu”alisema Mangalo.
Nahodha huyo aliongeza kuwa wachezaji wote wana ari na morari nzuri na kwamba taarifa zilizokuwa zikisambaa za wao kugoma kutokana na madai ya mishahara si kweli kwani tayari wamelipwa stahiki zao na kusisitiza kuwa leo lazima wafanye kweli.
Kwa upande wake Straika wa timu hiyo,Innocent Edwine alisema kwa sasa mechi zote zilizobaki ni muhimu sana kwao na si Yanga pekee,hivyo kila mchezo wanahitaji pointi tatu.
“Kwa sasa hakuna cha kushinda mchezo mmoja,tuna kazi ngumu kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kuanzia mchezo wa kesho (leo) ili kufikia malengo yetu”alisema Straika huyo.



0 Comments