JUMAPILI iliyopita, Klabu ya Yanga ilifanya uchaguzi mkuu kwa kuchagua viongozi wapya ambao wataiongoza klabu hiyo kwa kipindi cha miaka minne.
Viongozi ambao walichaguliwa kuongoza klabu hiyo ni pamoja na mwenyekiti, Dkt. Mshindo Msolla, makamu mwenyekiti, Fredrick Mwakalebela na wajumbe nane.
Viongozi hao watakuwa hapo kwa miaka minne na walipokea vijiti vya uongozi uliopita uliokuwa chini ya mwenyekiti, Yusuf Manji, makamu mwenyekiti, Clement Sanga na wajumbe ambao wote walijiuzulu kwa nyakati tofauti.
Ndoto ya wanachama wa klabu hiyo imeweza kutimia kwa kupata viongozi wapya jambo ambalo walikuwa wakilipigania kwa muda mrefu ili kuona klabu yao inakaa katika mstari mzuri.
Kwa sasa viongozi hao wapya wameingia madarakani na wanatakiwa kuanza kazi yao mara moja na hii ni kutokana na hali ya klabu hiyo ilivyo kwa sasa.
Inafahamika kuwa hali ya Yanga siyo nzuri kiuchumi ndiyo maana wanachama walikuwa wanapambana kwa nguvu zote kuona wanatimiza malengo yao ili timu yao ifanye vizuri.
Tunafahamu wakati wa kampeni kulikuwa na makundi mengi ambayo yalijitokeza kutoa sapoti kwa wagombea ambao walitaka washinde, lakini mwisho wa siku wapo walioshinda na wengine kushindwa.
Ili kuwa na Yanga moja, wale walioshindwa wanapaswa kuwaunga mkono walioshinda, isitokee kuwa na makundi tena wakati uchaguzi umekwisha na viongozi wamepatikana.
Itapendeza kuona kundi lililokuwa likimsapoti Dkt. Jonas Tiboroha ambaye alikuwa akiwania nafasi ya mwenyekiti na kushindwa, likaendelea kutoa sapoti kwa viongozi walioingia madarakani.
Kwa sasa wanachama wa Yanga mnapaswa kuwa kitu kimoja katika kuhakikisha mnatoa sapoti kwa viongozi wenu bila ya kujali wakati wa kampeni ulikuwa kundi gani.
Yanga imekuwa katika hali mbaya, hilo mnalifahamu, ukiangalia timu imepoteza nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa huu unakwenda msimu wa pili kitu ambacho zamani hakikuwepo.
Ni vizuri mkakaa chini na kuweka mikakati yenu na kushirikiana na viongozi ambao mmewachagua ili kuifikisha Yanga pale mnapopataka.
Pia ni vyema mkashirikiana na viongozi kujadili suala la mabadiliko ndani ya klabu yenu kwani hilo kwa sasa halikwepeki hata kidogo, hivyo shirikianeni kuijenga Yanga mpya ambayo itakuwa na mabadiliko.
Na sio vibaya kuiga kama walivyofanya watani zenu Simba ambao mabadiliko yao yameanza kuonekana kuzaa matunda kwa kiasi kikubwa, hivyo kazi kwenu.
Cha msingi kuweni kitu kimoja kama Yanga na wapeni ushirikiano viongozi wenu kwa manufaa na maendeleo ya klabu yenu, hakika miaka minne hii itakuwa ya furaha na maendeleo ndani ya Yanga.
Sasa ni wakati wa kuijenga Yanga imara na kurejesha heshima ya klabu ndani na nje ya mipaka ya Tanzania ambayo ilikuwa imepotea kwa miezi kadhaa kutokana na sintofahamu iliyokuwepo.
Kila mwanachama, shabiki na mdau aelekeze macho yake mbele ili kusaidia kuiboresha Yanga ili iimarike na kurejesha soka la ushindani na ushirikiano huo unapaswa kutolewa pia kwa klabu nyingine ambazo zinashiriki Ligi Kuu ya Bara na zile za chini ili kujenga misingi imara ya soka letu. Kila la Kheria viongozi wapya Yanga.
0 Comments