Windows

Ushindi wa Simba waitesa Yanga Ligi kuu



WANAUME wamerudi. Simba imerudi penyewe. Imerudi kileleni tangu ilipofanya hivyo kwa muda mfupi Agosti mwaka jana na kuziacha Azam na Yanga zikipokezana kabla ya Yanga kukaa jumla hadi jana Jumatano iliposhushwa kibabe.


Simba imerejea kileleni baada ya kuifumua Coastal Union kwa mabao 8-1 iliyoshuka Uwanja wa Uhuru, ikiwa na uchovu wa safari kwani iliingia jijini Dar es Salaam muda mfupi ikitoka Tanga huku Emmanuel Okwi na Meddie Kagere kila mmoja akipiga hat trick.


Hicho kilikuwa kipigo kikubwa zaidi katika Ligi Kuu msimu huu, lakini kikiwa cha pili kwa Wagosi miaka ya karibuni kwani April 18, 2015 ilipasuliwa 8-0 na Yanga na kushuhudiwa Amissi Tambwe akitupia mabao manne pekee yake.


Hat trick ya Okwi ilikuwa ya pili kwake msimu huu na kuwa kinara, baada ya awali Alex Kitenge kufunga dhidi ya Yanga wakati akiichezea Stand United, huku Fullu Maganga wa Ruvu Shooting na ile ya Salim Aiyee wa Mwadui kila mmoja akifunga yake msimu huu.


Okwi alifunga hat trick yake ya kwanza dhidi ya Ruvu Shooting walipoitungua mabao 5-0 na jana alitupia ya pili wakati Simba ikiiangamiza Coastal Union na kuandika rekodi ya msimu.


Katika pambano hilo lililokuwa la upande mmoja Okwi alifunga mabao yake dakika ya 11, 20 na 47 akitumia uzembe wa mabeki na kipa wa Coastal, huku bao la kufutia machozi la Wagosi likiwekwa kimiani na Raizin Hafidh dakika ya 35 kwa juhudi zake binafsi.


Kipindi cha pili Simba walionekana kucharuka zaidi na kuikimbiza Coastal kabla ya Meddie Kagere kufunga hat trick yake ya kwanza Ligi Kuu Bara kwa mabao ya dakika ya 69, 75 na 83, huku Hassan Dilunga na Clatous Chama wakitupia mengine.


Mabao hayo matatu kwa Kagere yamemfanya afikishe mabao 20 na kuzidi kuwaacha mbali washambuliaji wa timu nyingine, huku Okwi akifikisha mabao 14 akiwa sambamba na nahodha kwake, John Bocco ambaye jana alikosa mchezo wa nne kutokana na kuwa majeruhi.


Licha ya Coastal kujitutuma, Simba ilionekana haitaki utani kwa kutumia kila nafasi waliyopata na kuinyamazisha timu hiyo ya Tanga ambayo ilimiliki mpira kwa asilimia 25 tu dhidi ya 75 za Simba, huku ikipiga kona sita dhidi ya tisa za Simba.


Simba ilitengeneza mashambulizi mengi kupitia upande wa kushoto ambapo alikuwa anacheza Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Rashid Juma, lakini mashambulizi mengine yalipita upande wa kulia kwa Nicholas Gyan na Clatous Chama.


Wekundu hao walienda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-1 katika dakika 45 za kwanza baada ya mwamuzi Jonesia Rukyaa kupuliza kipyenga. Dakika 46, kiungo fundi Chama alipiga krosi nzuri ndani ya boksi ambayo mabeki wa Coastal walishindwa kuokoa na kumkuta Okwi aliyepiga shuti la kuzungusha lililokwenda kugonga mwamba na kutinga nyavuni.


Dakika 65, Simba walifanya mabadiliko kwa kumtoa Rashid Juma na kuingia Hassan Dilunga.


Mabadiliko hayo ambayo Simba waliyafanya yalionekana kuimarika zaidi na kuanza kushambulia na dakika 68, walifanya shambulizi ambalo lilimkuta Kagere ambaye alipiga shuti la chinichini na kipa Abdallah kulipanguwa na kuwa kona. Kona hiyo iliyokwenda kupigwa na Chama dakika 69, Kagere anaiunganisha kwa kichwa na kuifungia Simba bao la nne.


Dakika 72, Simba walifanya mabadiliko alitoka Okwi aliyefunga mabao matatu na kuingia Adam Salamba mwenye mabao manne mpaka sasa kwenye Ligi Kuu Bara akiifungia Simba. Dakika 75, Kagere alionesha tena makali yake baada ya kupokea pasi ya kupenyezewa na kupiga shuti la chinichini ambalo lilikwenda moja kwa moja nyavuni na kuiandikia Simba bao la tano.


Mpaka dakika 78, Simba ilifanya mabadiliko mengine ya kumtoa Said Ndemla na kuingia Mohammed Ibrahim ‘Mo Ibrahim’ walikuwa mbele kwa mabao 5-0.


Mabao matatu aliyofunga Kagere katika mechi na Coastal Union, yanamfanya kutimiza mabao 20, msimu huu katika mbio za kuwania zawadi ya mfungaji bora msimu huu.


Mabadiliko hayo ya Simba yalionekana kuongeza nguvu ya kushambulia kwani dakika 81, Mo Ibrahim aliyeingia kipindi cha pili alipiga pasi nzuri ndani ya boksi iliyomkuta Dilunga na kuifungia Simba bao la sita.


Simba hawakuishia hapo kulisakama lango la Coastal Union na dakika 83, Kagere aliifungia Simba bao la saba, ambalo linakuwa bao lake la 20, msimu huu kuifungia Simba akivunja rekodi ya mfungaji bora msimu uliopita Okwi. Dakika mbili za nyongeza kabla ya mechi kumalizika Simba walizitumia vyema kwa kuwafunga Coastal Union bao la nane kupitia kwa kiungo Chama ambaye linakuwa bao lake la tano msimu huu.


MTIBWA YABANWA


Mjini Manungu, mkoani Morogoro Mtibwa Sugar ikiwa nyumbani ilishindwa kufurukuta mbele ya JKT Tanzania kwa kulazimishwa sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Manungu Complex, huku kipa Benedict Tinocco akilazimika kujilaumu kwa makosa yake.


Katika mchezo huo, Jaffary Kibaya aliifungia Mtibwa mabao yote dakika ya 34 na 65, huku Mwinyi Kazimoto na Abdulrahman Mussa kufunga kwa upande wa JKT katika dakika ya 63 na 75.


Nayo Prisons ikiwa jijini Mbeya ilitoka suluhu na Ndanda kwenye pambano jingine lililpopigwa Uwanja wa Sokoine.


Post a Comment

0 Comments