Windows

Uongozi mpya Yanga waanza kusuka kikosi

YALE majembe yote Mwinyi Zahera aliyodai anataka yatue Yanga ili kuhakikisha msimu unaokuja kikosi hicho kinakuwa moto wa kuotea mbali, majina yao yameshatua mezani mwa uongozi mpya.

Tayari Yanga wameshapata uongozi mpya chini ya Mwenyekiti wake, Dk Mshindo Msolla, baada ya kukaa muda mrefu bila uongozi hiyo ikimaanisha kuwa ndiyo kwanza kazi inaanza.

Uchaguzi uliomweka madarakani Dk Msolla ulifanyika Jumapili iliyopita katika ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Jeshi Oyesterbay, jijini Dar es Salaam.

Alipotembelea ofisi za DIMBA zilizopo Sinza Kijiweni mapema mwezi wa pili mwaka huu, Zahera alisema anahitaji fedha za usajili zisizopungua shilingi bilioni 1.5 ili kupata wachezaji wenye hadhi ya kuichezea klabu hiyo.

Alisema ameshazungumza na baadhi ya nyota wa nje ya nchi na kilichobakia ni utekelezaji tu na uongozi huo mpya umemwahidi kwamba atapatiwa kila anachokihitaji.

Akizungumza kabla ya kuingia madarakani wakati wa kampeni, Dk. Msolla alisema, atahakikisha anampa Zahera fedha zote anazozihitaji ili kukijenga vizuri kikosi hicho.

“Pesa yote anayoitaka Mwinyi Zahera ataipata, naahidi mbele yenu na kama atahitaji zaidi ya Sh bilioni 1.5 atapatiwa,  lakini kubwa zaidi pesa yote atapewa yeye mwenyewe Zahera,” alisema Dk. Msolla kwenye kampeni zake.

Baada ya kura kuhesabiwa na kushinda, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, naye alirudia kauli hiyo akidai Zahera atapatiwa mzigo wote anaoutaka ili kukijenga kikosi imara.

Kigogo mmoja wa Yanga ambaye ameingia madarakani kwenye uchaguzi huo, ameliambia DIMBA Jumatano kwamba tayari wanayo baadhi ya majina ya wachezaji wanaotakiwa na Zahera hivyo wanasubiri tu muda ufike wafanye utekelezaji.

“Ni kweli yapo baadhi ya majina ambayo tumepewa kwa ajili ya usajili, sisi kama viongozi kazi yetu ni utekelezaji na hilo ninaamini tutalifanya kwa asilimia zote kwani ndivyo tulivyoahidi kwenye kampeni zetu,” alisema.

The post Uongozi mpya Yanga waanza kusuka kikosi appeared first on KWATA UNIT SPORTS & ENTERTAINMENT.



Post a Comment

0 Comments