NA SALEH ALLY
INAWEZEKANA watu ambao wamekuwa wakisema maneno kadhaa kuhusiana na tuhuma za utoaji rushwa wanakuwa hawajui madhara ya kile ambacho wanakizungumza.
Unaposema timu fulani inapendelewa, maana yake inatoa rushwa, kwa kuwa hakuna kupendelewa bila ya kuwa na kile ambacho unatoa ili upendelewe.
Suala la Simba inapendelewa, limechukua nafasi kubwa hasa baada ya kikosi hicho kuonyesha kuna kila dalili kitachukua uongozi wa ligi na ikiwezekana kubeba kombe.
Baada ya hapo, tumeanza kusikia Simba inapendelewa, Simba inabebwa jambo ambalo hatuwezi kulikubali kama wadau kuona kuna timu inabebwa kuelekea kubeba ubingwa.
Kama ni kweli, kuna kila sababu ya kuchukuliwa kwa hatua kulikomesha hilo ili kuwa na ligi ambayo ni ya haki bin haki na hata tukipata bingwa awe wa haki. Fair Game, inaongeza ubora kama wanaoshinda watakuwa wamepatikana bila ya upendeleo.
Kupendelea maana yake ni rushwa maana huwezi kusema mwamuzi kaipendelea timu fulani bila ya kuwa na chembechembe za rushwa. Sote tunapaswa kupiga vita masuala ya rushwa katika soka na lazima tupambane nayo ili kutengeneza heshima ya mchezo huo na kujenga maendeleo.
Kama mpira unategemea rushwa, kamwe hauwezi kuwa na maendeleo kwa kuwa wasio na uwezo watashinda kutumia fedha. Sasa ni wakati mzuri wa mapambano hayo kwa kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imeonyesha ilivyo karibu na tayari kushirikiana na wanaotaka kuukoa mpira.
Wale ambao wamekuwa wakilalamika, kwamba Simba inapendelewa au timu fulani inapendelewa, huu ndio wakati sahihi kabisa. Wakati wa kwenda na kueleza ushahidi wa kile walichonacho ili kumaliza utata huu ambao unaichafua Ligi Kuu Bara.
Vizuri kusiwe na mihemko na visingizio, vizuri kwenda Takukuru na kuwaeleza ili kutoa ushirikiano kwao nao waifanye kazi yao vizuri. Haitakuwa sahihi kuendelea kulalamika vijiweni na kujenga hisia kwa baadhi ya wadau kuwa kuna timu inayopendelewa.
Maana yake ni hivi, siku waamuzi wakikosea kwa Simba itakuwa wamewapendelea, wakikosea kwa timu nyingine inaonekana ni makosa ya kibinadamu. Tunapaswa kuifuta hii kwa kuwaeleza ukweli tulionao Takukuru na huu ndio wakati mwafaka wa kufanya hivyo.
Acheni kuzungumza tu kama kasuku, kusema maneno mitaani na kujenga hisia ambazo huenda zinaweza siziwe sahihi. Kama ni sahihi, basi Takukuru kwa kuwa ni watalaamu, wanaweza kufanya vizuri zaidi kazi yao kitaalamu kutokana na taarifa zenu ambazo zinapaswa kuwa na ukweli.
Lazima tukubali, kuendelea kusema maneno bila ya kuwa na uhakika ni kuendelea kuwaadhibu Simba kwa lazima na kuwavunja nguvu huku tukijua au kuona wanafunga mabao sahihi. Haiwezekani wao wakifungwa ndio iwe haki, wakishinda, wamependelewa.
Takukuru wanapaswa kuungwa mkono na kupewa shukrani kutokana na wepesi wao katika hilo kwa kuwa wamesema wameanza kufanya uchunguzi lakini wamesisitiza na kuwakaribisha wale ambao wamekuwa wakilalamika, kwamba sasa ni wakati mwafaka wa kupata hizo taarifa waendelee kuzifanyia kazi kitalaamu.
Pamoja na hivyo, niwasisitize wale wote ambao wamekuwa wakisikia tuhuma hizi kuhusiana na timu kupendelewa, pia hawapaswi kuhukumu. Badala yake wachunguze kwa kuangalia mechi za Simba bila ya kuwa na hisia kabla ya kupata majibu.
Ziangalie mechi za Simba, mpira unaonekana na kwa kuwa una uwezo wa kuona jibu pia utalipata. Usiangalie ukiamini ya kuambiwa, sasa maana au faida ya kuangalia ni ipi?
Kwa yule ambaye umeona, pia vizuri upate nafasi ya kuangalia badala ya kukubali kulishwa maneno ili mradi.
0 Comments