MABOSI wa Simba walipata mshtuko baada ya kuishuhudia timu yao ikicheza mechi mbili mfululizo bila kufunga bao hata moja na kuambulia alama moja tu na fasta wakaamua kufanya jambo ambalo liliwapa mzuka nyota wao na kuinyamazisha Mtibwa Sugar.

Mabosi hao wameamua kuwamwagia mamilioni ya fedha nyota wao kama njia ya kuwapa mzuka wa kuvuna alama tatu kwa kila mchezo kati ya zilizosalia ili kuimaliza Yanga ambao imekuwa ikiwawekea kauzibe kuutangaza mapema ubingwa wao wa pili mfululizo.
Simba imesaliwa na mechi nne kwa sasa baada ya juzi kuinyoosha Mtibwa Sugar mabao 3-0 na ushindi huo ulichagizwa na ahadi ya mabosi hao wa Msimbazi kwa kina Meddie Kagere, John Bocco, Emmanuel Okwi, Clatous Chama na nyota wengine kwamba kwa sasa bonasi ya ushindi imetoka Sh 10 milioni hadi Sh 20 milioni ili wabebe ndoo yao.
Ahadi hiyo ilianza kufanyiwa kazi na nyota hao baada ya kuigonga Mtibwa na sasa wanasubiri kuwafanyizia Ndanda watakaotua Uwanja wa Uhuru kisha Singida United ugenini, Biashara United na mechi ya mwisho ni dhidi ya Mtibwa Sugar mjini Morogoro.
Kama hujui ni kwamba tangu kuanza kwa msimu huu nyota wa Simba kila wanaposhinda mechi ya ligi walikuwa wanapewa Sh 10 milioni, ili wagawane kama motisha tofauti na mishahara yao, ila unaambiwa katika mechi tano kuanzia ya juzi wanavuta mara mbili.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori aliliambia Mwanaspoti kikosi chao kina zaidi ya wachezaji saba ambao ni majeruhi ambao wamewakosa kipindi hiki ambacho wamekuwa na ratiba ngumu ya ligi kucheza mechi kila baada ya siku mbili.
Magori alisema wachezaji wengi wameonekana kucheza muda mrefu na kuchoka uongozi umeliona hilo na ili kuhakikisha wanafanya vizuri na kufikia malengo yao wameweka motisha wa pesa zaidi ili wachezaji kushindana zaidi na kufikia malengo ya timu.
“Mechi zilizobaki motisha na posho zitakuwepo ili wachezaji wetu kushindana zaidi ili kumaliza kwa kutetea taji, tayari tumewaambia kilichobakia ni wao kupiga kazi tu,” alisema.
Simba ililirejea kileleni baada ya kuifunga Mtibwa, imekuwa ikichuana na Yanga katika mbio za ubingwa na hasa baada ya kupoteza alama tano mbele ya Kagera Sugar na Azam FC ambapo katika michezo minne iliyosaliwa nayo inahitaji alama tano kuwa bingwa.
Kwa sasa ina pointi 85 kutokana na mechi 34, wakati Yanga ina alama 83 zilizozalishwa na mechi 36 na kama Yanga itamaliza kwa ushindi itafikisha alama 89 ambazo Simba inaweza kuzipata katika mechi mbili tu kama itashinda moja na kutoka sare nyingine.
KIKOSI CHA CAF
Katika hatua nyingine Magori alikiri kuwepo kwa changamoto katika soko la usajili hasa kwa nyota wa kimataifa ambao pia huwa wanawindwa na klabu kubwa Afrika ambazo hutenga dau nono, lakini hata wao wamejipanga kuwa na kikosi imara cha CAF.
Magori alisema kuna baadhi ya wachezaji waliowaona katika timu kubwa Afrika na waliamini watawapata, lakini wamesajiliwa kwingine baada ya kuwekwa mzigo mkubwa, ila hawakata tamaa kwani wamejipanga kuwasapraizi mashabiki wa klabu hiyo.
“Uongozi unapambana kuhakikisha unafanikiwa kuwapata wachezaji ambao wataweza kuisaidia timu kwa mechi za ligi ya ndani na za kimataifa, sio kama tuliowakosa ndio wametuvunja nguvu, hapana hatujaanza usajili,” alisema.
Alisema kwa namna klabu yao ilivyojipanga na hasa baada ya kupata changamoto hizo na walivyoona ushiriki wao wa Ligi ya Mabingwa msimu huu walivyoishia robo fainali, wamejipanga kushusha majembe ya maana ambayo yataibeba timu msimu ujao.