Windows

Simba Yamuachia Beki Atue Yanga

IMEFAHAMIKA kuwa beki wa kati, Salim Mbonde ni mchezaji huru tangu msimu uliopita kutokana na kuondolewa kwenye orodha ya wachezaji waliosajiliwa klabuni hapo. Beki huyo, hayupo na timu hiyo tangu msimu uliopita ikiwa ni mara baada ya kupata majeraha ya goti na kumsababishia kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu.

 

Mbonde alijiunga na Simba kwenye msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar mara baada ya mkataba wake wa kuichezea timu hiyo kumalizika akisaini mkataba wa miaka miwili. Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Ijumaa imezipata, beki huyo jina lake liliondolewa kwenye usajili wa msimu huu baada ya kuwepo makubaliano ya pande mbili kati ya Mbonde na uongozi wa Simba, hivyo hivi sasa ni mchezaji huru anayeruhusiwa kusaini klabu nyingine ikiwemo Yanga.

 

Mtoa taarifa huyo alisema jina lake liliondolewa kutokana na majeraha ya muda mrefu yaliyokuwa yanamuandama katika timu hiyo kabla ya uongozi kukubaliana kuliondoa jina kwenye usajili na badala yake kubakisha mkataba wa ajira pekee, akiendelea kupokea mshahara wa kila mwezi ambao unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

 

“Kikanuni Mbonde siyo mchezaji halali wa Simba, kwani yeye tayari tulikuwa tumemuacha katika usajili wetu tangu msimu uliopita na huu hayupo, hiyo ni baada ya kufikia makubaliano mazuri kati yake na viongozi wa Simba.

 

“Tulikubaliana kuliondoa jina lake katika usajili wa ligi na tubakishe mkataba wa ajira pekee tukiendelea kumlipa mshahara, kwani hata kama angebaki asingekuwa anacheza kutokana na majeraha ya muda mrefu yaliyokuwa yanamuandama.

 

“Anaendelea kuchukua mshahara wa kila mwezi anaendelea kulipwa na Simba pekee hadi mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema: “Ni kweli Mbonde hayupo kwenye usajili wa msimu huu wa Simba, yalikuwepo makubaliano kati yake na uongozi katika kuliondoa jina lake katika usajili huo.” Alipotafutwa Mbonde kuzungumzia hilo, simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa kwa muda mrefu.

 

SPOTI HAUSI: AUSSEMS Kumkosa NIYONZIMA Simba SC

The post Simba Yamuachia Beki Atue Yanga appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments