LIGI Kuu inaelekea ukingoni huku Mnyama akiendeleza vichapo dhidi ya wapinzani wake, na mbaya zaidi kwa watani wake ni kumtoa kileleni Yanga baada ya mchezo wa Jumatano alipoishushia Coastal Union kipigo cha mbwa-koko cha mabao 8-1 kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Kichapo hicho cha Coastal Union kimeweka historia mbili mpaka sasa kwenye Ligi Kuu msimu huu, moja kuzaa ‘hat-trick’ mbili, pili kuzalisha kichapo kikubwa zaidi.
Vipigo vingine vikubwa vilivyotokea kabla ya mauaji ya Simba kwa Coastal, ni Simba kuilaza Alliance 5-1, kisha kumchapa Ruvu Shooting 5-0, Mbeya City akambwaga 4-1 African Lyon, Azam akajipigia 4-0 dhidi ya Mbao FC na KMC akashinda 5-1 dhidi ya Prisons.
Katika mchezo wa Jumatano mashabiki wa Simba walishuhudia nyota wao wakiondoka uwanjani na mipira miwili baada ya ‘hat-trick’ ya Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.
Hata hivyo, ‘hat-trick’ hizo si jambo jipya kwenye Ligi Kuu ya Bara kwani Amis Tambwe ndiye baba lao tangu alipotua nchini msimu wa 2013/14 kwa kuwa na ‘hat-trick’ nyingi zaidi kufiia sasa.
AMIS TAMBWE
Nyota huyo kutoka Burundi msimu wa kwanza anatua nchini kwenye kikosi cha Simba akitokea Vital’O FC alipiga ‘hat-trick’ ya kwanza wakati Simba wakiilaza Mgambo Shooting mabao 6-0 kwenye mzunguko wa nne wa msimu wa 2013/2014.
Mkali huyo hakuishia hapo kwani Februari mosi, 2014 Tambwe aliisaidia Simba kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 mbele ya JKT Oljoro msimu ambao timu hiyo kutoka Arusha ilishuka daraja, japo katika mzunguko wa kwanza Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na Simba kumaliza nafasi ya tatu ikiwa na alama 38 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Mbeya City na Yanga kumaliza ligi ikiwa nafasi ya pili kwa alama 56 huku Azam ikiwa mabingwa kwa alama 62.
HATARI TUPU
Msimu uliofuata Tambwe alitimkia Yanga ambako aliendeleza moto kama kawa licha kuachwa na Simba akionekana ameishiwa makali.
Alipiga ‘hat-trick’ mbili zote zikitengenezwa ndani ya mwezi mmoja.
Tambwe alianza kupiga ‘hat-trick’ walipoilaza Coastal Union 8-0 Aprili 8, hivyo kichapo cha wiki hii cha 8-1 mbele ya Simba kwa Wagosi kinaendeleza rekodi za vichapo vikubwa wanavyokumbana navyo.
Aprili 27 mwaka huo huo ikiwa ni wiki mbili baadaye Wanajangwani hao waliichapa Polisi 1-4, Tambwe akitupia tena ‘hat-trick’ na kuisaidia Yanga kubebwa ubingwa, huku yeye akitimiza ‘hat-trick’ nne ndani ya misimu miwili, huku kikiiacha Polisi ikishuka daraja.
AWEKA REKODI
Msimu wa pili akiwa Yanga (2015/16) aliweza kuandika ‘hat-trick’ nyingine mbili kwenye msimu huo na kuisaidia Yanga kubeba ubingwa kwa alama 73 na kuiacha Azam ikiwa na alama 63 ikishika nafasi ya pili kwenye kwenye msimamo wa TPL.
Tambwe aliandika ‘hat-trick’ yake ya tano wakati Yanga wakiilaza Stand United 4-0 kisha akatupia ‘hat-trick’ yake ya sita wakati chama lake likiilaza Majimaji FC bao 5-0. Kipenzi cha Simba, Okwi baada ya kutupia ‘hat-trick’ dhidi ya Coastal, amefikisha ‘hat-trick’ tatu, na ana kazi ya ziada kuifikia rekodi ya Tambwe.
HAT-TRICK ZA OKWI
Okwi alifunga ‘hat-trick’ yake ya kwanza katika ushindi wa Simba wa 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, straika huyo raia wa Uganda akipiga bao nne peke yake siku hiyo Agosti 26, 2017 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Straika huyo wa timu ya taifa ya Uganda alitupia ‘hat-trick’ yake ya pili wakati wakiichabanga Ruvu Shooting 5-0 kwenye Uwanja wa Taifa Oktoba 28, 2018.
Na akakamilisha ‘hat-trick’ yake ya tatu juzi Mei 8, 2019 katika ushindi wa 8-1 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa katika mechi ambayo wageni waliwasili siku hiyo hiyo ya mechi kwa basi baada ya kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 332 wakitokea Tanga.
MSIMU HUU
Hadi sasa tumeshuhudia ‘hat-trick’ sita zikifungwa msimu huu, tatu kutoka Simba ambazo zimetengenezwa na nyota wake, Okwi akipiga mbili na Kagere moja.
Alex Kitenge ambaye ndiye mchezaji wa kwanza kupiga ‘hat-trick’ katika Ligi Kuu ya Bara msimu huu wakati chama lake la Stand United likicheza dhidi ya Yanga kupitia mabao yake ya dakika 15, 59 na 90 japo walilala kwa mabao 3-4.
Januari 6, mwaka huu Salum Aiyee naye alifunga ‘hat-trick’ ya pili katika Ligi Kuu ya Bara wakati timu yake ya Mwadui iliposhinda 4-0 dhidi ya Kagera Sugar. Jumamosi ya Machi 2, 2019 Ruvu Shooting ilimlaza Mwadui 6-2 na Fully Maganga akapiga hat trick pia.
Jumatano wiki hii idadi ya ‘hat-trick’ 6 za TPL ilikamilika baada ya Simba kushinda 8-1, Kagere na Okwi wakituzwa mpira kila mmoja.
0 Comments