


PAZIA la Ligi Kuu Tanzania Bara linatarajia kufungwa kesho kwa timu zote 20 zinazoshiriki ligi hiyo kushuka dimbani katika viwanja tofauti nchini.
Ligi hiyo iliyoanza Agosti mwaka jana, imekuwa na matukio mbalimbali yaliyojitokeza kubwa likiwa ni ukata kwa klabu nyingi kutokana na kukosa mdhamini mkuu kama ilivyozoeleka.
Kwa muda mrefu, Simba na Yanga wamekuwa ni watawala wa ligi hiyo kutokana na kuwa washindani wakubwa, hali inayochangiwa na idadi kubwa ya mashabiki wao.
Hata hivyo, licha ya Yanga kukomaa na kuongoza ligi kwa muda mrefu, msimu huu imekuwa haina makali kama ilivyokuwa misimu iliyopita kutokana na kukabiliwa na hali mbaya kiuchumi.
Pamoja na hali mbaya kiuchumi, klabu hiyo pia ilikuwa haina uongozi wa kueleweka kutokana na viongozi wake wa juu kujiuzulu kwa nyakati tofauti.
Kitendo cha Yanga kukabiliwa na ukata, matatizo ya uongozi tangu msimu uliopita, imeshindwa kuchuana na Simba katika suala la usajili na kuifanya timu hiyo kuwa na kikosi kidogo.
Kwa kipindi chote hicho Wanajangwani hao walibuni kila mbinu ya kuifanya timu yao kuendelea kumudu mechi pamoja na kusajili wachezaji wasiokuwa na majina makubwa, lakini waliwasaidia kuleta ushindani ukizingatia kocha mkuu wa timu, Mwinyi Zahera, alikuwa mhimili wa kuwajenga wachezaji kiushindani.
Moja ya mbinu ambayo kikosi hicho cha Jangwani ilitumia katika kuhakikisha wanamudu kucheza mechi zote za ligi na kuwahudumia wachezaji, ni kupitisha michango kwa wanachama wake.
Wanayanga wamekubaliana na hali hiyo ya kuchangia timu hadi kipindi hiki ligi inapoelekea ukingoni na mafanikio yake yameonekana kwa sababu hakuna hata siku moja kikosi kilishindwa kusafiri kwenda kucheza mechi.
Ikumbukwe kuwa licha ya Yanga kuitwa watembeza bakuli, lakini waliweza kusafiri kwa ndege katika baadhi ya mikoa wakati wa kucheza mechi zao.
Kama klabu hiyo ilivyofanikiwa kusafiri na kumudu mechi za ligi na kuwaacha midomo wazi mashabiki wengi wa soka wakijiuliza kuwa iweje timu yenye njaa inaongoza ligi na inasafiri kwa ndege? Ndivyo itakavyoshtua katika usajili wa kipindi hiki.
Kutokana na wazo la kocha wake, Zahera la kutaka wanachama wachangishane fedha za usajili kupokelewa na kila mdau wa klabu hiyo kwa kuundwa kamati maalumu ya michango, ni wazi kuna kitu kikubwa kitatokea.
Hali inayodhihirisha kuwa klabu ya Yanga imejipanga kuchuana na mahasimu wao Simba katika usajili kipindi hiki, ni tetesi za majina ya wachezaji wanaodaiwa kutaka kutua katika timu hiyo.
Pia kitendo cha kumwongezea mkataba kiungo wao, Papy Tshishimbi ambaye alikuwa anafukuziwa na baadhi ya timu, ni dhahiri kutakuwa na kitu kikubwa kinakuja.
Licha ya Tshishimbi kuongezewa mkataba, kuna wachezaji wa nje tayari wameshatua kujaribu bahati yao katika timu hiyo, huku Zahera akiwaaminisha mashabiki wa Yanga kuwa atafanya usajili mkubwa.
Kwa taarifa ya fedha ambazo Wanayanga wanadaiwa kuchangangishana kama ni kweli zimepatikana, klabu hiyo ina uwezo wa kung’oa mchezaji sehemu yoyote kwa sababu tayari uongozi wa kuaminika umepatikana.
Kwa hali hiyo ni kuashiria kuwa licha ya Simba kufanikiwa kutetea ubingwa wao msimu huu, wajipange wakifahamu mahasimu wao wanarejea katika ushindani.
Wekundu wa Msimbazi hao wasibweteke na mafanikio waliyopata bali waendeleze mapambano, kwani wasipokuwa makini wanaweza kupigwa bao na Yanga.
Ikumbukwe kuwa hakuna kinachofanikisha usajili wa wachezaji wazuri katika klabu yoyote, zaidi ya fedha ambazo tayari Yanga wameshatenga dau lao.



0 Comments