Windows

Simba shangwe kama lote tu

LICHA ya uchovu wa kucheza mechi mfululizo na wakiwa ugenini kukabiliana na Singida United katika mechi ya Ligi Kuu Bara, unaambiwa huko Msimbazi kwa sasa shangwe ni kama lote kwa wachezaji na mashabiki wakihesabu saa tu kabla ya kulitia tena taji mkononi.
Ndio, Simba imeifuata Singida ikihitaji sare yoyote ili kutangaza ubingwa kabla ligi haijamalizika, kwani idadi kubwa ya mabao iliyonayo hata kama wapinzani wao wa jadi, Yanga watashinda mechi zao na kuzifikia pointi ilizonazo, Simba itabeba ndoo.
Singida iliyo chini ya Kocha Fred Felix ‘Minziro, inaingia kwenye mchezo huu ikiwa nafasi ya tisa na alama zake 45 inataka kuicheleweshwa Simba kutwaa ubingwa, lakini wapinzani wao wameapa leo lazima kieleweke Namfua.
Simba ina pointi 88 na mabao 74 ya kufunga, imeanza kushangilia mapema ushindi kwa kuamini kikosi chake hakijawahi kupoteza hata alama moja achilia mbali kufungwa na Singida tangu timu hiyo irejee kwenye ligi msimu uliopita.
Kama kuna kitu kinaifanya Simba ianze kuchekelea ubingwa ni makali ya safu yake ya ushambuliaji ambapo nyota wake watatu, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na John Bocco wametengeneza jumla ya mabao 52 kati ya 74 iliyofunga timu hiyo.
Katika mechi ya duru la kwanza Singida ilifumuliwa mabao 3-0, wakati msimu uliopita ilipoteza 4-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam , kabla ya kwenda kulala tena 1-0 nyumbani na kuonyesha walivyo wateja wa kudumu wa Msimbazi.
Hata hivyo, Kocha Minziro aliyeshiriki kuipandisha msimu uliopita kabla ya kupigwa chini, alisema Simba isitarajie mteremko kwani, hawataki kugeuzwa ngazi ya kuwapa ubingwa wa mapema wakiwa Namfua
Naye Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema wanaingia katika mchezo huo wakiwa na uhakika wa kutwaa ubingwa kwani hawaoni sababu ya kushindwa kupata japo alama moja, huku akitamba kuwa na michezo miwili zaidi mkononi ni hazina ya faida kwao.
Aussems alisema kwa vile watani zao Yanga wamebakiwa na mechi mbili, bado haoni tabu kwao kwa vile anaamini katika mechi zote tatu walizonazo alama moja wataipata na kukamilisha malengo yao ya kutetea taji msimu huu.
“Tunafahamu tunacheza na timu isiyo na rekodi nzuri dhidi yetu, lakini katika michezo kama hii inayotoa maamuzi ya ligi huwa inabadilika na tunaamini kutakuwa na ushindani, tunalifahamu hilo na tumejipanga kuhakikisha dhamira yetu inatimia,” alisema Aussems.
Nyota wa Simba wametamba kuwa licha ya uchovu walionao, lakini watashuka Namfua wakiwa na morali ili kupata ushindi na kuwapa raha mashabiki wao ambao wamekuwa wakiwaungwa mkono mwanzo mwisho na kuwapa nguvu.
Mkurugenzi wa Singida, Festo Sanga alisema kwa motisha yoyote ambayo wachezaji wao wanaitaka watawapatia ili kuhakikisha Simba hawapati hata hiyo pointi moja ambayo itawafanya wao kuwa katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa msimu huu.
“Kwetu haiwezekani misimu miwili yote Simba wanatufunga katika michezo minne, uongozi tumejipanga na tumewapa motisha wachezaji na benchi la ufundi ili kwenda kuvunja mwiko dhidi ya Simba ambao tumeonekana hatuna rekodi nao nzuri dhidi yao,” alisema Sanga.
Mara baada ya mchezo huo wa leo, Simba itageuza kurejea jijini Dar es Salaam kesho Jumatano ili kuwahi pambano lake la kimataifa la kirafiki dhidi ya Sevilla kisha kuisubiri Biashara United itakayocheza nayo wikiendi hii na baadaye kuifuata Mtibwa Sugar Jumanne ijayo ili kumaliza mechi za Ligi Kuu kwa msimu huu.

Post a Comment

0 Comments