

Mbeya. Simba imeendelea kusaka ubingwa baada ya kuichapa Prisons kwa bao 1-0 na kupunguza pengo la la pointi baina yake na Yanga.
Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi alilofunga bao pekee dakika ya 11, akitumia vizuri kukosa mawasiliano kati ya kipa wa Prisons, Aaron Kalambo na mabeki wake kwa kuwapiga chenga na kufunga goli hilo kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Okwi amefikisha mabao 11 katika ligi hiyo msimu huu, akiwa na kumbukumbu ya kufunga mabao 20 msimu uliopita.
Simba imefikisha pointi 78 baada ya kucheza mechi 30 na ipo nafasi ya pili, huku Yanga kesho itacheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Lipuli inaongoza kwa pointi 80.
Yanga iko mbele kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya Simba ikiwa imecheza mechi 34. Ushindi wa Simba unaongeza presha katika mbio za kuwania ubingwa dhidi ya kwa Yanga.
Yanga Alhamisi itacheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Biashara United ugenini mkoani Mara wakati Simba itavaana na Coastal Union Jumatano, Dar es Salaam.
Endapo Simba itaifunga Coastal Union itafikisha pointi 81 na kuiondoa kileleni Yanga kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu.
Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema timu yake ilikuwa na michezo 6 ndani ya siku 17, lakini anashukuru wachezaji wake kwa kutoa matokeo mazuri katika michezo hiyo licha ya ratiba hiyo ngumu kwao.
“Nashukuru leo tumeshinda mchezo mgumu kwetu kwani haikuwa rahisi kushinda kutoka na hali halisi ya uwanja na baada ya ushindi huo wa mapema kikosi change kilijimarisha zaidi upande wa ulinzi, kesho tunaondoka Mbeya kwa ajili ya kujiandaa na michezo mitano iliyopo mbele yetu,”alisema Aussems
Kocha Msaidizi wa Tanzania Prisons, Ramadhani Katumba alisema kilicho changia timu yake kupoteza mchezo kwenye uwanja wake wa nyumbani dhidi ya Simba imetokana na wachezaji kuwa na uchovu wa mchezo uliyopita dhidi ya Yanga uliyochezwa jijini Dar es salam Ijumaa iliyopita.
Katumba alisema timu yake ilimiliki mpira kwa nafasi kubwa ila walishindwa kutumia nafasi ambazo walikuwa wanapata kutokana kukosa utulivu wanapo karibia langoni.
“Tumetoka kucheza na Yanga Dar es salam na wakati tunarudi tulipata ajali na wachezaji wakawa na uchovu hivyo kukabili hali ya hewa ya Mbeya ikatusumbua wakati huo wenzetu walishafika siku nyingi, hivyo ni baadhi ya vitu vilivyochangia na unajua mtu ukitoka safarini ukapata ajari mawazo yanakuwa ni mengi ila namshukuru Mungu mpira umechezwa vizuri Simba wamepata bahati baada ya makosa ya beki wetu kutegeana na kipa na kupelekea wapinzani wetu kushinda,” alisema Katumba.
Prisons: Aaron Kalambo, Michael Mpesa, Leons Mutelemwa, Nurdin Chona, Vedastus Mwihambi, Jumanne Nimkaza, Salum Kimenya, Ezekiel Mwashilindi, Adam Adam Ramadhani Ibata na Ismail Kada.
Simba: Aishi Manula, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Erasto Nyoni Yusuph Mlipili, James Kotei, Clatous Chama, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere Emmanuel Okwi/Jonas Mkude na Haruna Niyonzima/Hassani Dilunga.
Aussems aliongeza kuwa kitu kizuri ni kuaondoka Mbeya na alama sita ambazo kuzipata ilikuwa siyo kazi rahisi kwani timu alizokuwa anakabiriana nazo zinaujua mpira vizuri.




0 Comments