

Msanii wa muziki wa kizazi kipya 'bongo fleva' Ali Kiba na Mwanasoka nyota wa Tanzania Mbwana Samatta anayekipiga KRC Genk, mabingwa wa ligi kuu ya Ubelgiji, wameandaa kampeni ya #Nifuate ambayo itahitimishwa kwa tukio la mchezo wa kirafiki utakaofanyika uwanja wa Taifa Juni 02 jijini Dar es salaam
Tamasha hilo litahusisha mchezo wa kirafiki kati ya Timu Kiba na Timu Samatta ambapo kila mmoja amechagua wachezaji wa timu yake wanaojumuisha watu wa makundi mbalimbali wakiwemo wasanii, wanamuziki, wanasiasa, wanasoka wanaosakata kabumbu sasa na hata wale waliostaafu
Viingilio katika mchezo huo ni Sh.2000 kwa viti vya mzunguko, eneo maalumu yani vip B ni Sh.5000 huku maalumu zaidi ikiwa Tsh Sh. 20,000
Nifuate ni kampeni maalumu imeanzishwa na mastaa hao kupitia taasisi yao ya Samakiba yenye lengo la kuungana na wadau wengine ili kwa pamoja waiguse jamii kwenye maeneo mbalimbali.
Katika uzinduzi wa kampeni hizo, Samatta alisema watatumia mchezo huo kama ilivyokuwa msimu uliopita kuchangisha fedha ambazo zitarudi kwenye jamii kutatua changamoto mbalimbali
"Nianze kwa kusema shukrani kwa Watanzania wote ambao wamelipokea hili vizuri tangu msimu wa kwanza hadi hivi sasa ambapo wengi wanaonekana kuguswa nalo.
"Lengo letu ni kuirudishia jamii na safari hii tutajikita wenye mambo matatu, ambayo ni kutoa misaada kwa yatima, kusaidia walemavu na kusaidia wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu," amesema Samatta.
Naye Ali Kiba amesema wameamua kutumia nafasi walizonazo kufanya Tamasha hilo ambapo kile kitakachopatikana chote kitarejea kwenye jamii



0 Comments