

Turin, Italia. Supastaa wa Juventus, Cristiano Ronaldo amedaiwa kuitaka klabu hiyo kumsajili Mohamed Salah wa Liverpool kwenye dirisha lijalo la usajili.Mabingwa hao wa Italia wanataka kukiboresha kikosi chake wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa rasmi ili kuwa na nguvu baada ya kuboronga kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya licha ya kunyakua Serie A kwa msimu wa nane mfululizo.
Mastaa kama Mauro Icardi, Matthijs de Ligt na David de Gea ni miongoni mwa wachezaji wenye majina makubwa waliyowekwa kwenye orodha ya timu hiyo, wakati Mo Salah jina lake likitajwa zaidi kwa siku za karibuni.
Na sasa kumekuwa na ripoti kwamba Ronaldo ameuambia uongozi wa Juventus kuhakikisha wanamchukua winga huyo wa kimataifa wa Misri ili kwenda kuifanya timu hiyo kuwa na mastaa watupu. Juventus tayari imeshamnasa Aaron Ramsey bure kutoka Arsenal, lakini wakati ikijiandaa kumpoteza Paulo Dybala wanajiandaa kuziba pengo lake kwa kumbeba Mo Salah.



0 Comments