


STRAIKA nyota wa Azam, Donald Ngoma amekiri kuchemsha katika msimu wake wa kwanza akiwa na timu hiyo akidai kuzidiwa mbinu na mabeki wa Yanga ambao wamemtibulia kutimiza malengo aliyojiwekea msimu huu.
Ngoma, aliyejiunga Azam akitokea Yanga msimu huu ameshindwa kuwatungua mabosi wake hao wa zamani na kudai ameshindwa kutimiza lengo lake la kuisaidia timu yake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ngoma alisema mipango yake ya kuifunga Yanga msimu huu imegonga mwamba na amewamwagia sifa mabeki wa timu hiyo kuweza kumudu mbinu zake na kumfanya ashindwe kufikia malengo aliyokuwa ameyakusudia.
“Nimefanya kazi na Kelvin Yondani, Andrew Vincent ‘Dante’, ni mabeki wanaonifahamu vizuri wanajua ubora wangu na mapungufu yangu ukiachana na hao pia kuna wachezaji wengine wengi waliopo Yanga nimecheza nao misimu miwili, hivyo wamenidhibiti.”
“Nikikutana na Yanga nacheza kama ninavyocheza na timu nyingine huwa sihofii chochote lakini juhudi zangu zimekwama kwa vile nyota wengi wananijua, hivyo kunitibulia kila kitu nilichokipanga kwa msimu wangu wa kwanza Azam,” alisema Ngoma.
Straika huyo alisema bado hajakata tamaa kwa kuamini kuwa msimu ujao anaweza kufanya makubwa kwa vile kila siku kiu yake ni kuona anafika mbali na kutimiza malengo na hasa tangu alipokuja Tanzania akitokea kwao Zimbabwe.
Ngoma amemaliza msimu akiwa na mabao 11, ingawa ameshindwa kuitungua Yanga kwani mechi ya duru la kwanza timu yake ililala 1-0 kwa bao la Mrisho Ngassa na juzi Azam ilishinda mabao 2-0 kwa mabao ya Daniel Amoah na Mudahiri Yahya.



0 Comments