KUNA wakati unaweza kutamani kurudisha nyakati nyuma lakini siyo jambo rahisi. Kamwe huwezi kurudisha siku zilizopita. Lakini ni rahisi sana kuvuta kumbukumbu ya kilichotokea nyuma. Mwanamuzuki wa Bongo Fleva, Rehema Chalamila ‘Ray C’ amenikumbusha nyuma. Amenikumbusha kwenye enzi zake. Miaka ya katikati mwa 2000. Wakati akiwa Kiuno Bila Mfupa kwelikweli! Kipindi ambacho alikuwa ghali zaidi kwenye Bongo Fleva miongoni mwa wasanii wenzake wa kike. Wakati huo haikuwa rahisi kumuona mara kwa mara.
Nyakati hizo, Ray C alikuwa na foleni ya watangazaji wa vipindi vya Bongo Fleva waliotaka kufanya naye mahojiano. Shoo kila wikiendi, ndani na nje ya Bongo. Namzungumzia Ray C wa ‘Nimezama’. Achana na wimbo huo kuna pini nyingine inaitwa ‘Mahaba ya Dhati.’ Unakumbuka wakati huo?
Nyimbo nyingine alizopata kutesa nazo Ray C ni pamoja na Uko Wapi, Na Wewe Milele, Wanifuatia Nini, Mapenzi Matamu, Sogea Sogea na kibao cha miaka ya hivi karibuni cha Mama Ntilie alichoshirikishwa na wasanii Gelly wa Rymes akiwa na AT.
Ray C asiyekauka kwenye chati mbalimbali za wiki kwenye redio mbalimbali. Ilikuwa ukisikiliza Bamiza Top 20 (Magic FM) utamsikia, Ladha 10 za Bongo (Radio One) utamsikia au ukifuatilia Top 20 (Clouds FM) lazima umsikie. Vituo vyote hivyo na vingine vilivyokuwa vikitesa wakati huo, alikuwa katika chati za juu zaidi.
Ladha ya Ray haikuwa ya kitoto. Kifupi Ray C alikuwa juu, kiasi kwamba alikuwa akisumbuana vikali na wasanii wa kiume. Ray C alikuwa akipeta katikati ya Jide, Dataz, Zay B, Stara Thomas na wengineo. Ushindani ulikuwa wa hali ya juu. Ilikuwa ni kawaida kwake kusafiri hadi China kwa ajili ya kurekodi video ya wimbo wake mpya. Kipindi kile, msanii kusafiri hadi nje ya nchi, tena sehemu kama China ilikuwa siyo jambo dogo.
Lakini Ray wa sasa amebadilika. Amepitia mengi hapo katikati ambayo sipendi kuyakumbusha maana sasa ni Ray mpya anayeishi nje ya nchi. Tofauti ni kwamba mtazamo, umaarufu, uwezo wa kuimba na mengine mengi ya wakati ule, hana tena kwa sasa.
Picha ndogo ni Ray C amepozi na msanii wa muziki nchini Marekani Ja Rule. Ni picha ya zamani hii. Ray C mwenyewe aliposti picha hii kwenye ukurasa wake wa Instagram juzi Jumatano, Mei 15, wakati akisherehekea kumbukizi ya kuzaliwa kwake.
Kiukweli nikivuta kumbukumbu zangu nyuma, nimemtamani sana Ray C yule wa zamani arudi leo hii, lakini ndiyo hivyo huwezi kurudisha nyakati nyuma. Komando Jide aliyeanza naye muziki enzi zile, bado yupo kwenye game hata kama hana moto mkali kama wa wakati ule. Kuna kitu cha kujifunza hapo.
RAY C ANAWEZA KURUDI
Kunahitajika juhudi kubwa, kujituma, kujinyima na nidhamu ya hali ya juu ili Ray C aweze kurudi kwenye zama zake. Ni ngumu, lakini inawezekana akarudi hata kama ni kwa kiasi.
Wakati nikiwa kwenye tafakari hiyo, nikamkumbuka msanii mwingine wa Bongo Fleva ambaye aliwika kiasi kwamba, akaonekana kama angeweza kuziba pengo ya ladha ya burudani iliyoachwa na Ray C. Msanii huyo ni Rachel ambaye jina lake halisi ni Winfrida Josephat. Rachel ni zao la Jumba la Vipaji Tanzania ‘THT’ ambaye mapigo yake, uvaaji wake na hata uimbaji wake ulikuwa ukishabihiana na wa Ray C wa wakati ule.
Aliingia kwa kasi kwenye game na wengi waliamini ‘upele umepata mkunaji’, lakini ghafla Rachel naye amepotea! Kama yupo, basi amenyamaza kimya. Kati ya vibao vyake ni pamoja na ‘Nashukuru Umerudi’. Kiukweli nami nitashukuru sana siku akiamua kurudi kwenye game.
TUMJADILI NANDY KIDOGO
Nandy ni msanii mwingine wa kike kwenye Bongo Fleva ambaye anafanya vizuri kwa sasa. Uwezo wake siyo wa kupapasa. Kifupi anajua anachokifanya. Kwa mbali nikimwangalia, namuona Ray C mpya ndani ya Nandy. Siyo Ray C kwa maana ya fleva za kufanana, hapana. Uwezo wake wa kuimba, kutawala jukwaa na namna anavyoishi kwenye jamii ya mastaa. Kuna wakati alipitia kwenye ukakasi kidogo, lakini tangu pale amekuwa makini zaidi.
Nandy anaweza kuwa juu zaidi ya alipo akitaka. Akitengeneza nidhamu zaidi, kujituma zaidi, ubunifu zaidi na akiwa na menejimenti nzuri zaidi au aliyonayo ikiongeza juhudi zaidi, tutamshuhudia Nandy mwingine mkali zaidi. Kama vipi Nandy chukua nafasi ya Ray C wa zamani, maana uwezo huo unao. Ni suala la kuamua tu.
The post NAMTAMANI RAY C HUYU ! appeared first on Global Publishers.
0 Comments