Windows

Nahimana kumfuata Ndayiragije Azam FC



UONGOZI wa klabu ya Azam umeanza mikakati ya kuboresha kikosi chao baada ya kuanza mazungumzo na kipa wa KMC ya Kinondoni, Jonathan Nahimana, ili ajiunge na timu hiyo katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Usajili wa kipa huyo unakuja baada ya uongozi wa Azam kuanza mazungumzo na kocha mkuu wa KMC, Etienne Ndayiragije, ambaye ametoa masharti ya kusajiliwa kwa kipa huyo anayeichezea timu ya Taifa ya Burundi.

Taarifa za uhakika zilizolifikia BINGWA jana kutoka kwa kigogo mmoja wa Azam, zinaeleza kwamba mazungumzo kati ya Ndayiragije na uongozi wa klabu hiyo yamefikia hatua nzuri ambapo sasa wanafikiria kuzungumza na Nahimana ili achukue nafasi ya Razaq Abalora.

Alisema uongozi wa Azam ulianza kufanya mazungumzo na aliyekuwa kipa wa Yanga, Beno Kakolanya, lakini sasa umesitisha mpango huo kutokana na kocha huyo kuwapa masharti ya kuhitaji huduma ya Nahimana.

“Kila kitu kinakwenda vizuri, mambo yakikamilika kipa huyo atakuwa miongoni mwa wachezaji wa Azam kwa sababu kocha anayekuja anahitaji huduma yake,” alieleza.

Hata hivyo, BINGWA lilimtafuta Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’, kuthibitisha taarifa hiyo lakini alieleza kwamba bado hawajaanza mchakato wa kusajili wachezaji wa nje hadi hapo watakapopata kocha mkuu.

Popat alisema mchakato wa kutafuta mirithi wa Hans van der Pluijm, unaendelea na muda ukifika wataweka hadharani jina la kocha aliyepita baada ya kufanyia kazi CV za wale walioomba kazi.

“Kwa sasa usajili bado hivyo siwezi kuzungumzia taarifa hizo, kikubwa mashabiki wavute subira na kusubiri mchakato wa kutafuta kocha na baada ya hapo tutamsikiliza anahitaji wachezaji wa aina gani ili usajili uanze,” alisema Popat.

Post a Comment

0 Comments