MWENYEKITI wa Klabu ya Yanga, Dk Mshindo Msolla, amesema kuwa mafanikio aliyoyapata mshambuliaji wao Mkongomani, Heritier Makambo yametokana na malengo na juhudi zake za kujituma ndani ya uwanja huku akiwataka wachezaji wengine kupitia kwake akiwemo nahodha, Ibrahim Ajibu.
Msolla alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache tangu wapokee ofa nne za mshambuliaji huyo kuhitajika na nchi mbili za Afrika na nyingine za Ulaya. Makambo Jumatano iliyopita alisafiri kwenda nchini Guinea kwa ajili ya kufanyiwa vipimo Klabu ya Horoya AC kabla ya kuanza mazungumzo na uongozi wa Yanga.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Msolla alisema kuwa mshambuliaji huyo ni mfano wa kuigwa kwa wachezaji wa Yanga kama wanataka kufanikiwa kama ilivyokuwa kwa Makambo ambaye yeye hakuwa anaweka migomo mbalimbali iliyokuwa inatokea kwenye timu hiyo.
Msolla alisema, Makambo ni mchezaji pekee mwenye ofa nyingi ndani na nje ya Yanga kwa wachezaji wa Ligi Kuu Bara ikiwemo kuhitajika na moja ya klabu za nchini Ubelgiji. Aliongeza kuwa, wachezaji hao wa Yanga akiwemo Feisal Salum, Papy Tshishimbi basi ni lazima wajitume ndani ya uwanja ili wazishawishi baadhi za klabu za ndani na nje ya Afrika ili kuwafuata na kuwanunua.
“Licya ya klabu ya Yanga kuyumba kidogo kiuchumi, lakini ni moja ya klabu kubwa inayofuatiliwa na mawakala mbalimbali kwa ajili ya kuwaangalia wachezaji na kuwafuata kwa ajili ya kuwanunua. Na ili mchezaji aonekane ni lazima ajitume na kuachana na baadhi ya mambo mengine, zaidi ni kucheza na kujituma na kuachana na mambo ya migomo pale mishahara inapocheleweshwa.
“Makambo hakuwa na mambo hayo ya ajabu ya kususia mechi mbalimbali za mashindano ikiwemo ligi, yeye alikuwa anafanya kazi vizuri katika timu na ndiyo sababu ya kufikisha idadi hiyo ya mabao 16 katika ligi na leo hii unamuona huyo anaondoka wakati wowote kwani tayari ana ofa nne zikiwemo za Ulaya, ipo moja ya klabu kutoka Ubelgiji nayo imeonyesha nia ya kumsajili,” alisema Msolla.
WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam
Masele Alivyozikwepa PINGU KAJA Mwenye
The post Msolla Ampa Mchongo Ajibu appeared first on Global Publishers.
0 Comments