


BILIONEA wa Simba, Mohammed Dewji, amewakata kilimilimi wapinzani wao wa jadi, Yanga, baada ya kutamka wazi kwamba kiungo wao fundi, Jonas Mkude, haendi popote.
Akitumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook, Dewji alitupia picha ya Mkude na kuandika: “Wanasimba msiwe na wasiwasi, Mkude haendi popote! Jumaah Kareem.”
Maneno hayo ya Mo Dewji, ni kama majibu kwa Yanga, ambao wamesema walishaanza mazungumzo na Mkude ili kumsainisha kwa ajili ya msimu unaokuja.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, ndiye aliyesema wameshaanza mazungumzo na Jonas Mkude, na muda wowote angesaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo, lakini kauli ya Mo Dewji ni kama imezima uvumi huo.
Taarifa zaidi kutoka Simba zinadai kuwa, Mo Dewji alimuita Mkude nyumbani kwake juzi usiku baada ya kumalizika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Sevilla ya Hispania na kuweka mambo sawa.
Mbali na Mkude, taarifa hizo zinadai kuwa, Mo Dewji ameanza rasmi kazi ya kuzungumza na nyota waliomaliza mikataba yao, ambao wapo kwenye mipango ya Kocha Patrick Aussems, wakiwamo Haruna Niyonzima, Erasto Nyoni, Emmanuel Okwi, Shomari Kapombe na Aishi Manula.
“Mo alikutana na Mkude jana (juzi) usiku nyumbani kwake, baada ya kumalizika mchezo dhidi ya Sevilla, ameanza rasmi kazi ya kuzungumza na wachezaji waliomaliza mikataba na wapo kwenye mipango ya Kocha.
“Hizi siku chache atamalizana nao wote, akiwamo Niyonzima (Haruna), Okwi (Emmanuel), Aishi Manula, Erasto Nyoni pamoja na Kapombe (Shomari),” alisema kigogo mmoja ndani ya Simba.
Alisema mpaka sasa wachezaji wa kigeni wenye asilimia kubwa ya kuonyeshwa mlango wa kutokea ni Asante Kwasi na Nicholas Gyan, huku akidai Zana Coulibaly ambaye mashabiki wamekosa imani naye akikingiwa kifua na kocha na huenda akaendelea kuwepo msimu unaokuja.



0 Comments