


KOCHA Mkuu wa Sevilla ya Hispania, Joaquin Caparos, amekisifia kikosi cha Simba kutokana na kiwango walichokionyesha katika mchezo wa kirafiki uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo wa kusisimua, Sevilla walishinda mabao 5-4, ikiwa ni baada ya kuwa nyuma kwa mabao 3-1 hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Caparos alisema kipindi cha kwanza Simba walicheza vizuri na kufunga mabao matatu, lakini mabadiliko aliyofanya yalimsaidia na kupata ushindi.
“Awali, tuliona mchezo ni rahisi, lakini tumecheza na timu ambayo ni nzuri, inapambana. Wamecheza mpira mzuri, kweli timu hii ni bingwa,” alisema.
Alisema Simba ina wachezaji wazuri ambao wapo imara, ambao walipambana kwa dakika zote 90 na kupata mabao manne.
Caparos alisema wamefurahi kucheza na timu kama ya Simba, kwani wamewapa burudani mashabiki waliojitokeza uwanjani kushuhudia mchezo huo.
Kwa upande wake, winga wa Sevilla, Quincy Promes, amewavulia kofia nyota wa Simba, Haruna Niyonzima, Meddie Kagere na John Bocco kwa kiwango kizuri walichokionyesha kwenye mchezo huo. “Awali nilikuwa siifahamu timu hii na wala sijawahi hata kuisikia, lakini tumekuja na tumecheza nao tumeona walivyocheza vizuri. Kuna wachezaji wazuri…yule aliyevaa jezi namba nane na 22 na 14, walicheza soka la kuvutia,” alisema



0 Comments