

ACHANA na sherehe zinazotarajiwa kufanyika Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro unaambiwa Ligi Kuu Bara inatarajiwa kufungwa kibabe, ambapo klabu nane zitakuwa kwenye vita nzito ya kufa au kupona katika kuwania kusalia kwenye ligi ya msimu ujao.Nd io, Simba itak uwa ugenini mjini Morog oro kumalizana na Mtibwa Sugar ikiwa tayari imeshabeba ubingwa mapema na leo ni kukabidhiwa tu, lakini Klabu za Biashara United, Kagera Sugar, JKT Tanzania, Mbao, Mwadui, Stand United, Prisons na Ruvu Shooting zinaombeana mabaya katika mechi zao ili zisiifuate African Lyon iliyoshuka daraja.
Hatma ya timu hizo itajulikana jioni ya leo Jumanne baada ya kipyenga cha mwisho cha kufungia msimu wa 2018-2019 ambao umekuwa na changamoto za kutosha ikiwamo ratiba iliyoyumba na vitimbi vingine vilivyosisimua hasa viporo vya kumwaga vya Simba.
Vita kubwa ipo kwenye pambano la Mbao na Kagera Sugar uwanjani CCM Kirumba, jijini Mwanza na ile ya JKT Tanzania na Stand United uwanjani Isamuhyo, jijini Dar es Salaam.
Kila timu inapambana kutoshuka daraja na mshindi atakuwa salama kusalia kwa msimu ujao, zitakazochemsha zitatoa mkono wa kwaheri ama kutupwa kwenye play-off ili kujiokoa mbele ya Pamba ya Mwanza na Geita Gold FC za Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Mbao ina pointi 44 na ikitoka sare au kupoteza mchezo huo itasikilizia matokeo ya mechi za Prisons (43), Ruvu Shooting (42) na Mwadui (41) ili kujua hatma yake.
Mwadui itakuwa mjini Shinyanga kuialika Ndanda, lakini hali waliyonayo Wakata Almasi hao ni kama vile ya Kirumba, ambapo Kagera yenye pointi 43 na Mbao lazima moja ishinde la sivyo itakayofungwa itasubiri miujiza ya kuibakisha msimu ujao.
Kocha Mkuu wa Kagera, Mecky Maxime alisema; “Tunajua umuhimu wa kushinda mechi ya kesho (leo), tuna dakika 90 za kubadili upepo, lazima tuzitumie kwa umakini.”
Kocha Msaidizi wa Mbao, Fulgence Novatus, alikiri timu yao kuwa katika kipindi kigumu, ila alisisitiza wachezaji wote wameandaliwa kisaikolojia ili kushinda.
Mwadui itakayoikaribisha Ndanda ni pambano litakalovuta hisia za mashabiki wa soka kwani wageni hawana cha kupoteza kwa vile wapo salama katika nafasi ya saba na alama zao pointi 48 wakati wenyeji yupo naafsi ya 19 na pointi 41 tu.
Straika wa Mwadui, Ditram Nchimbi anaumizwa na matokeo mabovu ya timu yake lakini anajipa matumaini ya kuwemo msimu ujao wa ligi kwa kuwataka wachezaji wenzake kupambana.
STAM HANA PRESHA
Kama ilivyo kwa timu nyingine za Kanda ya Ziwa, Biashara United nayo hatima yake ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao itajulikana leo ikiwa ugenini kucheza na Mbeya City ambao panga la kushuka haliwagusi.
Biashara ina pointi 44 inashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi hiyo,inahitaji ushindi ili kuwa na uhakika wa kushiriki ligi hiyo msimu ujao wakati Mbeya City imekusanya pointi 47 na kukaa nafasi ya nane.
Kocha wa Biashara, Amri Said ‘Stam’ alisema; “Kikubwa tumejiandaa kisaikolojia vijana wangu wanajua umuhimu wa mchezo wa huu, najua presha itakuwa kubwa kwetu lakini tutapambana kushinda na kujiweka nafasi nzuri mashabiki watuombee.”
Biashara imepewa Sh. 1.5 milioni kama motisha ili washinde dhidi ya City kwenye Uwanja wa Highland Estate ulioko Mbarali mkoani Mbeya.
Aliyewapa motisha hiyo ni Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, aliyesema ametoa kiasi hicho kwa wachezaji na benchi la ufundi ili kuhakikisha Mkoa wa Mara haupotezi timu ya Ligi Kuu msimu ujao.
Katibu wa klabu hiyo, Haji Mtete alisema mbunge alikabidhi fedha hizo juzi na anaamini wachezaji wake watafanya vizuri katika mechi yao hiyo.
“Mbunge amekuwa mdau mkubwa wa timu yetu na ameamua kutusaidia kiasi hicho cha fedha kama motisha ili kuongeza ari, kwani tukifungwa tutakuwa tumeshuka daraja,” alisema Mtete.
Alisema Prof. Mhongo amekuwa akijitolea kwa hali na mali tangu timu ikiwa daraja la kwanza na hatimaye Ligi Kuu na bado anaendelea kuisaidia na anatamani timu isishuke daraja, huku akisisitiza wana imani na ushindi kwani katika mechi ya kwanza walishinda 2-1.
ALLIANCE HESHIMA TU
Alliance inayoshiriki msimu wa kwanza katika Ligi Kuu, tayari ina uhakika wa kuwepo tena msimu ujao na kocha wake, Malale Hamsini akitaka kuweka heshima mchezo wao wa mwisho dhidi ya Ruvu Shooting utakaochezwa Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.
Ruvu Shooting bado wanapambana kujinasua kwani wana pointi 42 wakishika nafasi ya 18 kwenye msimamo wakati wapinzani wao wana pointi 47 wapo nafasi ya tisa.
Ushindi wowote au sare ya Alliance itawafanya Ruvu Shooting kushuka daraja msimu ujao jambo ambalo litafanya mchezo huo kuwa mgumu hasa kwa wenyeji hao.
Malale alisema mikakati yao ni kumaliza ligi wakiwa na pointi 50 hivyo watapambana kuhakikisha wanapata ushindi.
“Ni mchezo mgumu lakini tutapambana uzuri kikosi changu kipo kamili kikubwa tunahitaji pointi tatu kumaliza ligi na alama 50,” alisema Malale.
SIMBA SHANGWE TUPU
Wakati klabu nyingine zikiwa katika presha Simba yenyewe mashabiki wao wamekaa mkao wa shangwe kwani wanatarajia kuishuhudia timu yao ikikabidhiwa taji lao mjini Morogoro baada ya sherehe zao kutibuliwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa.
Viongozi wa Simba wa mjini Morogoro wakishirikiana na viongozi wakuu wamepanga kuupamba mji wa Moro rangi nyekundu na nyeupe wakati wakilitembeza taji lao, huku wale wa Kibaha wakiweka bayana mapokezi waliyoiandalia timu yao.
Simba imetwaa ubingwa kwa kufikisha alama 92 ambazo haziwezi kufikiwa kwani, Yanga iliyoongoza msimamo kwa muda mrefu msimu huu imemaliza nafasi ya pili ikiwa na alama 86 huku ikimalizana na Azam FC iliyopo nafasi ya tatu na alama zake 72.
KMC na Mtibwa Sugar zipo katika vita ya kuwania nafasi ya nne japo kila moja itakuwa kwenye uwanja tofauti kisaka alama tatu muhimu za kufungia msimu.
Makala zaidi za Ligi Kuu msimu huu zipo kurasa za ndani kwa toleo maalum.
IMEANDIKWA NA IMANI MAKONGORO, SADDAM SADICK, JAMES MLAGA NA MASOUD MASASI



0 Comments