WAKATI leo kikiwa ni chungu cha pili cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kauli ya staa wa muziki wa Afro-Pop, Nasibu Abdul almaarufu Diamond Platnumz kuwa hadi sasa amejenga misikiti si chini ya sita (6) na madrasa, imeibua gumzo kama lote, Risasi Mchanganyiko linayo.
Diamond au Mondi alitoa kauli hiyo wikiendi iliyopita alipokuwa akimjibu mmoja wa mashabiki wake.
CHANZO CHA YOTE
Chanzo cha yote ni posti ya video aliyoweka Mondi kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram ikimuonesha akicheza pool table na mmoja wa mameneja wake, Sallam SK almaarufu Mendez. Staa huyo aliyeachia wimbo mpya wa Inama akiwa na mwanamuziki mkali wa Rhumba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Fally Ipupa alikasirishwa na shabiki huyo aliyemnanga kuwa amelewa pombe mbele ya kamera na kuonesha umma waziwazi.
Kufuatia ‘komenti’ ya shabiki huyo ndipo Mondi akamtolea uvivu kama ifuatavyo na kuibua ishu hiyo ya misikiti na madrasa ambayo ndiyo ikazalisha mambo mengine;
diamondplatnumz: Home sweet home rooftop lounge na @sallam_sk now! virusividogo (shabiki): Kuna kufa, kuna kaburi na kuna Allah…na kuna siku utakutana naye, kumbuka hilo!
diamondplatnumz:@ virusividogo Mwenzio nina misikiti si chini ya sita na madrasa za kumwaga… sijui wewe umejiandaaje Muislam mwenzangu… Kauli hiyo ya Mondi ndiyo iliyoibua gumzo ambapo baadhi ya Waislam wenzake walimpongeza huku wengine wakimkosoa kwamba hicho ni kiburi cha utajiri na wala hapaswi kutangaza.
Walikwenda mbele zaidi kwa kumkosoa kuwa, hata kama amejenga idadi hiyo misikiti, alitoa kama sadaka ambayo akiitoa kwa mkono wa kulia hata mkono wa kushoto haupaswi kujua. “Diamond anapaswa kujua kuwa misikiti ni ya Mwenyezi Mungu, kama anatangaza kama vile amejijengea yeye, basi hana malipo yoyote kwa Allah.
“Allah hapendi mtu mwenye kiburi na hakika tunakumbushana kuwa sadaka bora ni ile itolewayo kwa kificho. “Sadaka inapaswa ikitolewa kwa mkono wa kulia, basi wa kushoto usijue. “Kuhukumu ni suala la Allah mwenyewe, sisi ni kukumbushana tu kwa njia za busara na kusameheana.
“Diamond aache kujidanganya kwamba akishajenga misikiti, basi anakuwa mtakatifu, anatakiwa kujua kwamba hata ajenge misikiti mingapi, Mungu cha kwanza anaangalia hiyo pesa aliyojengea msikiti au madrasa kwa sababu kama amejenga kwa pesa ya muziki, kisheria kwenye dini yetu muziki ni haramu, sasa ukijisifia kujenga misikiti kwa pesa haramu huoni kuwa hayupo sawa?
“Vyote hivyo unaweza kuwa navyo, lakini kama huswali ni kazi bure. Ni kama kwenda sokoni kisha ukanunua vitu halafu ukawa huna kapu la kubebea.
“Hata hivyo, kuwa na misikiti bila kumuogopa Allah ni kazi bure,” ilisomeka sehemu ya maoni mengi ya wakosoaji wa kitendo cha Mondi kutangaza kuwa na misikiti na madrasa. Hata hivyo, kwa upande wa pili wa shilingi, baadhi ya mashabiki wa Mondi walipongeza kwa hatua hiyo ya kujenga misikiti na madrasa. “Hongera kwa kujenga nyumba ya ibada Allah akujalie mahitaji ya moyo wako,” ilisomeka sehemu ya maoni ya kumpongeza Mondi.
SHEHE AFUNGUKA
Kufuatia mkanganyiko huo, Gazeti la Risasi Mchanganyiko lilizungumza na mmoja wa mashehe maarufu aliyeomba hifadhi ya jina ambaye alijibu kwa kifupi;
“Kwanza Diamond anakosa sifa za kuwa Muislam kwa sababu kisheria muziki ni kazi za kishetani na hata kuvaa kwake misalaba na nyimbo zake ni za kishetani.”
MISIKITI YA MONDI
Kufuatia ishu hiyo kuwa ‘hoti’ baadhi ya mashabiki wa Mondi walikuwa wakibisha kuwa hana idadi hiyo misikikiti hivyo gazeti hili lilizungumza na mameneja wake wawili, Said Fella na Hamis Taletale ‘Babu Tale’ ambapo kila mmoja alifunguka;
SAID FELLA
Kwa upande wake Fella alisema; Ni kweli Diamond ana misikiti mingi, lakini ili kujua iko wapi na wapi, hebu mcheki Babu Tale.”
Risasi Mchanganyiko lilimfikia Babu Tale ambapo alitaja misikiti ya Mondi sehemu mbalimbali hapa nchini;
“Ni kweli ana misikiti mingi. Kuna ambao upo Newala na mwingine upo Mtwara. Pia kuna mwingine Kibamba (Dar) ambao ataukabidhi chungu cha kumi na mwingine upo Kigoma.”
Gazeti hili linafahamu kuwa Mondi pia ana msikiti mkoani Morogoro, Iringa na Tandale jijini Dar.
BINTI ATESEKA MIAKA 6 KITANDANI/maumivu ya nyonga yalemaza mguu
The post MISIKITI 6 YA MONDI GUMZO! appeared first on Global Publishers.
0 Comments