Baba mmoja, Tatizo Japhet (37), mkazi wa Igurusi, Mbarali mkoani Mbeya, ametiwa mbaroni kwa kumuuza bintiye, Rose Japhet, mwenye umri wa miaka sita ili auawe na viungo vyake vitumike kujipatia utajiri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema leo, Mei 11, 2019 kuwa watu hao wanahusika na mauaji ya mtoto huyo ambapo mzazi huyo anadaiwa kulipwa Sh5 millioni na mfanyabiashara anayemiliki shule moja ya sekondari iliyopo Mbalizi, Wilaya ya Mbeya.
Kamanda Matei amesema Mei 3, mwaka huu, muda wa saa 3 usiku katika eneo la msitu wa Hifadhi wa Chimala-Mbarali mtoto huyo alikutwa ameuawa kwa kunyongwa kisha kukatwa kanyagio la mguu wake. Hata hivyo hukutaja ni mguu upi.
Amesema katika msako wa polisi, kanyagio la mtoto huyo lilikutwa limefukiwa eneo la Mbalizi wilaya ya Mbeya.
“Chanzo cha tukio hili ni tamaa ya kupata utajiri. Baba mzazi wa mtoto huyo alimtoa mwanaye huyo kwa mmiliki wa shule kwa malipo ya Sh5 milioni,” amesema Matei.
“Lengo auawe na kisha kanyagio la mguu wa kulia kupatiwa mfanyabiashara huyo apeleke kwa mganga ili amtengenezee dawa ya utajiri (ndagu), aweze kufanikiwa kwenye biashara zake za shule anayomiliki.”
Kamanda Matei amesema, mfanyabiashara huyo baada ya kuhojiwa alikiri kuhusika na tukio hilo na wanaendelea na uchunguzi wa kina pamoja na kumtafuta mganga aliyetarajiwa kupelekewa kiungo hicho kwa hatua zaidi za kisheria
0 Comments