Windows

MAN CITY YABEBA KOMBE LA FA, YAIPIGA WATFORD BAO 6-0

MANCHESTER City jana iliweka rekodi ya kutwaa mataji matatu katika msimu baada ya kuichapa Watford mabao 6-0 kwenye mechi ya fainali ya Kombe la FA iliyopigwa katika Uwanja wa Wembley. Timu hiyo ilinyakua Kombe la FA baada ya kuwa imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu England na Kombe la Carabao mapema msimu huu wa 2018/19.

 

Manchester City wamefuata nyayo za wapinzani wao wa jadi, Manchester United, ambayo ndio timu ya mwisho kutwaa mataji matatu katika msimu baada ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la FA kwenye msimu wa 1998/99.

Hata hivyo, Manchester City wamekuwa tofauti kidogo kwa kuwa wamechukua mataji matatu ya ndani ya England. Hii ni mara ya sita kwa Manchester City kunyakua Kombe la FA baada ya kutwaa kwenye misimu ya 1903/04, 1933/34, 1955/56, 1968/69 na 2010/11.

 

Wapinzani wao Watford walikuwa wametinga kwa mara ya pili katika fainali ya michuano hiyo, ambapo mara ya kwanza ikiwa msimu wa 1983/84.

Shujaa wa Manchester City alikuwa Raheem Sterling, ambaye alipiga mabao matatu `hat-trick’ kwenye mchezo huo. Mfungaji wa bao la kwanza la Manchester City alikuwa David Silva mnamo dakika ya 26 baada ya kupiga shuti akiwa pembeni ya goli baada ya kupokea pasi ya kichwa ya Sterling. Sterling aliiweka pazuri Manchester City baada ya kuongeza bao la pili katika dakika ya 38 baada ya kuujaza mpira uliodunda kwenye mstari wa goli baada ya kubetuliwa na mwenzake Gabriel Jesus.

 

Kevin de Bruyne, ambaye aliingia badala ya Riyad Mahrez, alifunga bao la tatu la Manchester City mnamo dakika ya 61 baada ya kupokea pasi ya Jesus, ambapo alimhadaa kipa wa Watford, Heurelho Gomes kama anataka kupiga shuti lakini akamzunguka na kufunga kiulaini.

 

Jesus alipachika bao la nne la City katika dakika ya 68 baada ya kupokea pasi ya De Bruyne, ambapo alikimbia na mpira ndani ya eneo la goli la Watford na kupiga shuti akiwa
na kipa Gomes mbele yake.

 

Sterling aliongeza bao la tano la Manchester City katika dakika ya 81 baada ya kupiga shuti lililogonga mwamba wa juu baada ya kumbabatiza kipa Gomes baada ya kupokea pasi ya Benardo Silva.

 

`Hat-trick’ ya Sterling ilikamilika katika dakika ya 84 baada ya kuunganisha wavuni krosi ya Bernado Silva aliyekuwa amepokea pasi ya De Bruyne. Watford, hata hivyo, watajutia nafasi mbili walizokosa kwenye dakika za mwanzo za mchezo huo.

The post MAN CITY YABEBA KOMBE LA FA, YAIPIGA WATFORD BAO 6-0 appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments