Windows

Makambo atengewa Sh228 million

SAWA msimu ujao wa kimataifa, Yanga ni kama haina chake vile kwani tayari tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika ilishaipoteza mbele ya Lipuli Iringa, ila hilo halijaufanya uongozi wa klabu hiyo kuacha kujipanga kukisuka upya kikosi chake kwa msimu ujao wa michuano ya ndani.
Lakini katika ya mipango yake hiyo ya kufanya usajili mzito habari mbaya ni kwamba moja kati ya klabu za Afrika kuhitaji saini ya straika wake matata, Heritier Makambo na kama kocha wake, Mwinyi Zahera atakubali, basi jamaa hatabaki Jangwani.
Taarifa ambazo uongozi wa Yanga unazifanya kuwa siri kubwa ni juu ya ofa hiyo ambayo imetua klabuni hapo hivi karibuni ikimtaka mshambuliaji huyo raia wa DR Congo, lakini Mwanaspoti limefanikiwa kupenyezewa bila chenga juu ya mchongo huo.
Bosi mmoja wa Yanga ameliambia Mwanaspoti, Makambo ana ofa ya sio kwenda kujaribiwa, bali ni kuuzwa, huku klabu hiyo (ikifichwa jina lake) ikitaka kutoa kiasi kisichopungua Dola 100,000 (zaidi ya Sh.228 milioni).
Dau hilo sasa lipo mezani kwa Yanga likisubiri kujua kipi kitaamuliwa na Kocha Zahera ambaye ndiye aliyemshusha nchini mwishoni mwa msimu uliopita akitokea kwao, DR Congo.
Hata hivyo, kitu pekee ambacho Zahera na mabosi wa klabu hiyo wanaweza kukitumia ni kusalia kwa mkataba wa mwaka mmoja ambapo kama wataendelea kuitingisha klabu hiyo inaweza kuongeza mzigo zaidi.
Bosi huyo (jina tunalo) alisema haoni kama Yanga itapata hasara kwa kuchukua kiasi hicho kutokana na klabu hiyo kutumia kiasi kidogo kumpata mshambuliaji huyo aliyetokea DC Motema Pembe baada ya kuvunja mkataba.
“Makambo anatakiwa na klabu moja sitaki kukutajia kwa sasa kwa vile mambo hayajakamilika na iko tayari kutoa kiasi cha Dola 100,000” alisema bosi huyo ambaye alihusika kwa kiasi kikubwa katika usajili wake.
“Tunachosubiri ni jibu na uamuzi wa Kocha Zahera ambaye kimsingi ndiye mwamuzi kiufundi, lakini kwa kiasi hicho au hata zaidi sioni kama ni shida kwa Yanga naona ni faida kwa kuwa tulimpata kwa bei rahisi kupitia mpango wetu wa kuepuka usajili wa gharama kubwa.
“Kwa sasa uamuzi upo kwa Zahera na hata uongozi mpya chini ya Mwenyekiti Dk. Mshindo Msolla kama watakubaliana sawa.”
Hata hivyo, aliongeza, licha ya ofa hiyo ambayo ipo wazi zaidi lakini wakala wa mchezaji huyo ambaye anaishi Afrika Kusini ana ofa tatu za majaribio za mshambuliaji huyo.
“Hiyo ni ofa ambayo imejitosheleza na tuliwaambia wasubiri kwanza amalize ligi kwa kuwa hatukutaka achanganyikiwe wakati ule tulipokuwa tunacheza mechi muhimu za Kombe la FA.
“Unajua wachezaji wa Kikongomani wanaposikia wanahitajika sehemu ni habari kubwa kwao, unaweza kuona hata uwezo wake uwanjani unapungua sasa tusubiri kuona kipi kitaamuliwa na uongozi.”
Makambo tangu atue Yanga msimu huu amefanikiwa kuifungia timu yake mabao 16 katika Ligi Kuu, huku akifunga mengine manne katika michuano ya Kombe la FA ambapo Vijana wa Jangwani waling’olewa hatua ya nusu fainali za Lipuli FC katika Uwanja wa Samora, Iringa.
Straika huyo pia ameweza kunyakua tuzo mbili mfululizo za Mchezaji Bora wa Miezi ya Novemba na Desemba na kuisaidia Yanga kukaa kileleni kwa muda mrefu kabla ya juzi Jumatano kushushwa na Simba.

Post a Comment

0 Comments