Windows

Kwani Mastaa hawa kwa Ferguson ingekuwa vipi hapo Manchester United

Mwanaspoti, Michezo, Michezo blog, Mastaa, Ferguson, ingekuwa, vipi hapo, Manchester United


TANGU ianzishwe, miaka 117 iliyopita, klabu ya Manchester United inajivunia rekodi ya kutwaa ubingwa wa EPL mara 20, FA Cup 12, Kombe la ligi tano, Ngao ya jamii 21, Ligi ya mabingwa mara tatu na Europa League mara moja.


Katika kipindi hicho, Mashetani wekundu, wamepitia kwenye mikono ya makocha 25, lakini ni ngumu kuitaja United, bila ya kulitaja jina la Mskochi Sir Alexander Chapman Ferguson.


Kati ya makocha wote 25, Ferguson ndiye aliyekaa Old Trafford kwa muda mrefu na kutwaa mataji mengi zaidi. Tangu atue pale Old Trafford, hakuna aliyekanyaga ‘Theatre of Dreams’, akaachwa salama.


Enzi za utawala wake, ulioanza 1986, akirithi mikoba ya mtangulizi wake, Ron Atkinson, mashetani wekundu walikuwa mashetani kweli, sio hawa wa sasa wanaofungwa 4-0 na Everton. Ile ilikuwa inabatiza kwa moto na maji!


Baada ya kukaa Old Trafford, kwa miaka 26 na kuweka makombe 38 kabatini, mwishoni mwa msimu wa 2012/13, Mskochi huyu alisema basi inatosha. Akakabidhi kijiti kwa David Moyes. Kuanzia hapo, Stori imekuwa tofauti.


Licha ya kusajili mastaa wakubwa, kutwaa ubingwa wa EPL, imekuwa ndoto. Ligi ya mabingwa imekuwa ni sawa na wazo la kumiliki kumjia kapuku. Lakini hivi umewahi kujiuliza, Ferguson angekuwepo, ingekuwaje kwa mastaa hawa?


ALEXIS SANCHEZ


Tuanzie wapi? Tuanze na mshahara na marupurupu inayomfanya Alexis kuingiza kiasi pauni milioni 28, ndani ya miezi 15, huku akiendelea kusugua benchi pale Old Trafford au tuanze na jinsi ujio wake ulivyowatikisa Marcus Rashford na Anthony Martial?


Vipi kuhusu hili la United kumsajili kama mbinu ya kuwadhibiti mahasimu wao, Manchester City? Kivyovyote vile, sidhani kama yangetokea kama Ferguson bado angekuwa Kocha, au tuseme kuwa, huenda hata ingekuwa nafuu kwa Sanchez, kwani angembadilisha.


FRED NA MEMPHIS DEPAY


Licha ya kuonesha kuimarika, lakini Fred bado hana tofauti kubwa na scott McTominay, na hapa niwe wazi kuwa Pauni milioni 52, ilikuwa ni matumizi mabaya ya fedha. Vipi kuhusu Memphis Depay, hata ni afadhali aliondoka.


Huyu nadhani walimharakishia majukumu, ambayo kwa umri wake, hakustahili kubebeshwa. Miaka 21, unampaje jukumu la kiutuzima la kulinda ngome la timu kubwa kama United, kama sio uonevu na tusi kwa wanaume kama Rio Ferdinand?


MARCOS ROJO


Unaweza ukahisi ni dharua, ashakum sio matusi, haijalishi ni namba gani, beki ya kushoto au beki ya kati, Marcos Rojo anakuwa na faida sana kwa United, akiwa nje ya uwanja kuliko anapopangwa kikosini.


Rojo aliyejiunga na United, sio yule Muargentina wa uliyemfahamu, akiwa Sporting Lisbon, nadhani hata wao walifurahi sana, United ilipoleta ofa ya kutaka huduma zake. Walijua wanachokiuza.


Pauni milioni 16, pamoja na Luis Nani, huu ulikuwa ni zaidi ya uzembe wa kufikiri. Sikatai kuna wakati aliwahi kuisaidia United, lakini Ferguson angekuwepo, mawili yangetokea, Rojo asingesajiliwa au angemsajili na kumsaidia kuwa bora zaidi ya alivyo hivi sasa.


ANGEL DI MARIA


Ni ngumu kusahau kuwa, Di Maria alikuwa sehemu ya kikosi cha United, msimu wa 2014/15, ambapo alionesha uwezo mkubwa, kabla ya majira ya baridi. Unakumbuka ushindi wa 5-3 walioupata dhidi ya Leicester City.


Hiyo ilikuwa ni moja ya mechi alizocheza kwa kiwango kikubwa kati ya mechi zake 10 za mwanzo, akiwa na jezi ya mashetani wekundu. Baridi ilipoingia, ikaja na majeruhi kapuni. Di Maria, hakusalimika. Kilichofuata ni Di Maria wa kawaida.


Haikumchukua muda akafunga safari kuelekea Paris, Ufaransa. PSG walizama mfukoni na kukamilisha dili, lililoiacha United na faida. Ni kweli alikuwa majeruhi, lakini chini ya utawala wa mtu kama Ferguson, Di Maria asingeachia aondoke.


NEMANJA MATIC


Hivi hii biashara ilifanywa na nani? Sidhani kama ni Ed Woodward. Sio kwamba Matic hana kiwango, lakini uharaka uliotumika kumuuza, unaweza ukakuthibitishia jambo. Chelsea walishajua huyu, hana jipya tena, wakaona isiwe tabu, wakachukua pauni zao 40 milioni.


ERIC BAILLY


Hapa patamu, unakumbuka sifa alizopewa na mashabiki wa United? Sawa kumsema Bailly sio haki, ukizingatia kuwa alikuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na Mourinho, akiwa na miaka 22 tu, akapiga shughuli kwelikweli.


Hivi sasa sijui kipi kimetokea. Ni sawa kama ilivyo kwa Rojo, majeruhi yamechangia mdororo wa kiwango chake, lakini mbali na hilo, Bailly hususan msimu huu, hajawa na jipya. Hivi ingekuwaje angesajiliwa na Ferguson?


JUAN MATA


Hivi United, walipomsajili Juan Mata, walitegemea angekuwa na msaada mkubwa? Akiwa Chelsea alikuwa moja viungo bora kwenye EPL, kila mtu alikuwa anamfananisha na David Silva. Alipotua Old Trafford, hakuwa na jipya. Makocha wanne wote wameshindwa kumsaidia.


Alipofunga bao dhidi ya Liverpool, kila mtu alianza kumwagia sifa, kiasi cha kushindwa kugundua kuwa, katika msimu mzima wa 2015/16, licha ya kucheza masaa 26 ya EPL msimu huo, Mata hakufunga bao wala kutoa asisti hata moja, zaidi ya kuunga kwa penalti.


HENRIKH MKHITARYAN


Unakumbuka akiwa Borussia Dortmund? Henrikh Mkhitaryan alikuwa anaivutia klabu yoyote. Alikuwa mashine balaa. Katika msimu wake wa mwisho, aliifungia Dortmund mabao 55, katika mechi 52. Kwa hili wala siwalaumu United.


Lakini Arsenal walikuwa wanawaza nini walipokubali kumsajili nyota huyu kutoka United? Ni sawa lakini kwa sababu hawana la kuwafanya wajute, maana afadhali ya Mkhitaryan kuliko huyo Alexis Sanchez.


LUKE SHAW


Kama kuna mchezaji aliyefanikiwa kuwaumbua wabaya wake, ni Luke Shaw. Kuna kipindi ukiachilia Jeraha la mguu, ambalo nusura limegharimu soka lake pia aliwahi kushtumiwa kunenepa hovyo. Haya yote yalimfanya aonekana hafai pale Old Trafford.


Hata hivyo, japo hajafanikiwa kurudisha makali yake, au kutimiza ahadi yake wakati akitua United, beki huyu wa kushoto, ameonesha uwezo mkubwa chini ya Ole Gunnar Solskjaer. Ndio kwanza ana miaka 23, kwa hiyo bado ana muda.


ROMELU LUKAKU


Alipokuwa Chelsea alitabiriwa kuwa mrithi wa Didier Drogba. Lakini haikuwa hivyo. Akaenda Everton, ambako alikuwa moto wa kuotea mbali. Kiwango chake kikaivutia Chelsea, ambao walitaka kumrudisha Darajani.


Katika vita hivyo, Man United walikuwepo. Wakafanikiwa kumshawishi kwenda Old Trafford, badala ya Chelsea. Pauni milioni 75, zikatumika kumsajili. Hata hivyo, kila mtu anaongea lake hivi sasa. Sijui nini imetokea, ila anachokifanya Lukaku (25), ni kurukaruka tu.


ANTHONY MARTIAL


Kwa sasa huyu ndio staa wa United. Licha ya kuonekana kuchoka katika siku za hivi karibuni, lakini kwa kiasi kikubwa, ameibeba United, akifunga asilimia 50 ya mabao yao msimu huu. Unaonaje angekuwa katika moja ya vikosi vya Ferguson, ingekuwaje?


Tangu mechi yake ya kwanza, alipojiunga na klabu hii, Mfaransa huyu, amekuwa moto wa kuotea mbali. Aliifunga Liverpool, katika mchezo wake wa kwanza. Kuna wakati, yeye Rashford na Lingard, walitengeneza utatu mtakatifu.


Amekuwa bora katika mechi kubwa, ikiwemo mechi ya nusu fainali ya kombe la FA, msimu wa 2015/16. Ana wastani mzuri wa kufunga bao, ambapo ni bao moja katika dakika 130. Kuna kipindi Mourinho alianza kumvuruga, lakini chini ya Ole, maisha ni matamu.


PAUL POGBA


Paul Pogba, mtukutu, mkorofi lakini miguu yake na moyo wake, ikiamua kufanya kazi kwa pamoja, utampenda bure. Katika mechi tisa za mwanzo za Ole Gunnar Solskjaer, Pogba alichangia mabao 13. Naam, huyu ni mashine ambayo inafanya kazi inapojiskia.


Mara ya kwanza, alisajiliwa na Ferguson, akiwa kinda. Kutokana na uchanga wake, Babu Fergie akamruhusu kuondoka. Baada ya kukua, Mourinho alitoa pauni milioni 100, kumrejesha Old Trafford, lakini akamfukuzisha Mourinho kazi.


Licha ya kumchezesha katika nafasi isiyo yake, chini ya Mourinho, Pogba alimaliza mwaka 2018, akiwa na mabao mengi na asisti za haja. Ni mmoja kati ya nyota watano ambao wamewahi kufanya hivyo.


ZLATAN IBRAHIMOVIC


Wakati akiwa Old Trafford, United ilitwaa mataji mawili. Hiyo ilikuwa ni msimu wa 2016/17. Wengine wanasema kuwa, uwepo wake, ulipunguza kasi ya mashambulizi, lakini ukweli usemwe, kwa umri wake wa miaka 35, alijaribu kwa kweli.


Alifunga mabao 28, na asisti 10, sio kitu cha kubeza kwa mchezaji wa umri wake. Hebu jiulize kama alifunga hayo mabao kwa umri huo, ingekuwaje angekuwa na miaka 25? Mbona Ferguson angefurahi.


ANDER HERRERA


Hivi tunahitaji kuwa na mjadala kuhusu uwezo wa Mhispania huyu. Kumjadili kwangu naona ni kumvunjia heshima kabisa. Ander Herrera amekuwa zaidi ya mchezaji tangu atue Old Trafford akitokea West Ham.


Rekodi hazidanganyi. Herrera na De Gea, ndio wachezaji pekee walioshinda taji la mchezaji bora wa klabu, tangu Alex Ferguson aondoke. Anapokuwa uwanjani, nuru ya United hung’aa zaidi.


Chini ya Ole Gunnar Solskjaer, Herrera anapokuwa uwanjani, United imecheza mechi 14, ikashinda 11, sare moja na kufungwa mara mbili tu. Ilipocheza bila Herrera (11), United imeshinda mechi tano, sare moja na kipigo mara tano.


Post a Comment

0 Comments