Kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino amejikuta akiangua kilio baada ya timu yake kuibua na ushindi wa mabao 3-2 ugenini dhidi ya Ajax na kutinga hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Baada ya dakika 90 za mchezo huo kumalizika, kocha huyo alikimbia hadi eneo la kuchezea uwanjani na alipiga magoti akiomba dua uwanjani hapo.
Pochettino alibubujikwa na machozi ya furaha huku akipongweza na wasaidizi wake pamoja na wachezaji.
Kocha huyo raia wa Argentina aliendelea kufuta machozi kisha kwenda kumpongeza nahodha wa timu hiyo, Hugo Lloris baada ya mchezo kukamilika, huku Ajax wakiwa wameng’olewa kwa goli la ugenini baada ya ushindi wa jana kuwafanya kuwa kuwa na uwiano wa mabao 3-3.
Mchezo wa nusu fainali ya kwanza Spurs walijikuta wakitandikwa bao 1-0 kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Pochettino baada ya kumalizika mchezo huo alizungumza mbele ya waandishi wa habari na kusema kwamba, ni jambo gumu kuelezea hisia zake kwa maneno.
Alisema katika maisha yake limekuwa jambo zuri kushuhudia kikosi chake kikitinga hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
0 Comments