Windows

KIULAINI: Simba kama inanawa ubingwa ligi kuu bara

USHINDI wa mabao 2-0 dhidi ya Ndanda FC juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, umeirahisishia Simba mbio za ubingwa wa Ligi Kuu kwani baada ya kutimiza pointi 88, sasa inahitaji pointi mbili tu katika mechi zake tatu zilizosalia ili itwae kombe.


Pointi hizo mbili zitaifanya ibebe rasmi ubingwa kwani itafikisha alama 90 ambazo hazitoweza kufikiwa na timu nyingine yoyote kwani Yanga wanaoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wana pointi 83 hivyo wakishinda mechi zao mbili zilizobaki watafikisha pointi 89.


Ushindi dhidi ya Ndanda ni kiashirio tosha cha kuamka kwa Simba ambayo iliyumba mechi mbili mfululizo za raundi ya 32 na 33 na ilifungwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar na kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Azam ingawa ilijitafakari kwa kushinda dhidi ya Mtibwa Sugar.




KAGERE SOMO LA KUJITAMBUA


Meddie Kagere amekuwa moto wa kuotea mbali msimu na kabla ya mechi dhidi ya Ndanda, alikuwa na mabao 20 ambayo yalimweka kwenye nafasi nzuri ya kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu na mabao mawili aliyofunga juzi yamemfanya afikishe ya mabao 22.


Kagere anafunga mabao hayo katika kipindi ambacho Simba inakabiliwa na ratiba ngumu ya kucheza idadi kubwa ya mechi mfululizo huku kundi kubwa la wachezaji wake wakionekana kuchoka lakini kwa Kagere licha ya changamoto hiyo, bado amekuwa akipambana kuibeba timu yake kwa kuifungia mabao muhimu yanayoamua mechi kama alivyofanya juzi dhidi ya Ndanda.

MLIPILI, MAYANGA DHAHABU





Mmoja wa wachezaji ambao wameonyesha kiwango bora msimu huu ni Vitalis Mayanga wa Ndanda FC ambaye amefunga jumla ya mabao 10.


Ana utulivu wa hali ya juu, anajiamini pindi awapo na mpira miguuni, ana uwezo wa kuwatoka mabeki, kupiga pasi za mwisho na kufunga. Haya amekuwa akiyafanya kwenye mechi dhidi ya timu kubwa na hata zile ambazo Ndanda wanacheza na timu za daraja la kawaida.


Ni mchezaji ambaye kama akiendeleza jitihada zake na kupata huduma sahihi, atapiga hatua kubwa siku za usoni.


Pia yupo beki Yusuph Mlipili wa Simba ambaye amekuwa akifanya vizuri katika mechi za hivi karibuni ambazo anapewa nafasi kutokana na kukosekana kwa Juuko Murshid na Pascal Wawa. Ana uwezo wa kutibua mashambulizi ya timu pinzani, hesabu sahihi pindi anapokabiliana na washambuliaji, ana uwezo wa kucheza mipira ya krosi, pia anaweza kupanga timu.




VITA YA KUSHUKA Kama kuna jambo linalonogesha Ligi Kuu msimu huu basi ni vita ya timu zinazopigania kubaki kwenye ligi hiyo na hadi sasa ukiondoa African Lyon iliyoshuka, bado haijajulikana nani wataungana naye chini, pia timu mbili zitakazocheza mechi za mchujo. Kutokana na utofauti mdogo wa pointi baina ya timu na timu, ni klabu sita tu ambazo hadi sasa zimeepuka kushuka daraja ambazo ni Simba, Yanga, Azam, KMC, Lipuli na Mtibwa Sugar lakini timu 13 zilizobaki ukiondoa Lyon ambayo imeshuka, hazina uhakika wa kubaki na namna zitakavyochanga karata zao kwenye mechi zilizobakisha ndivyo zinavyoweza kunusurika au kuzama.




SIMBA KURUDIA HISTORIA?


Msimu uliopita Simba ilitangazia ubingwa ikiwa hotelini huko Singida baada ya watani wao Yanga kupoteza mechi dhidi ya Prisons huko Mbeya ingawa Simba walikuja kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida United.


Safari hii wanaenda tena kucheza dhidi ya Singida wakihitaji pointi mbili tu ili watangaze ubingwa kwa kufikisha pointi 90. Ushindi dhidi ya Singida United leo Jumanne utawafanya waandike historia mpya kwa kutangaza ubingwa ndani ya mkoa mmoja mara mbili mfululizo. Kutoka kutangazia ubingwa hotelini hadi uwanjani, ni jambo linalosisimua mno.

Post a Comment

0 Comments