Kuivaa Mtibwa wakiwa na harufu ya ubingwa
ZAITUNI KIBWANA NA HUSSEIN OMAR
KITENDO cha kufungwa na Kagera Sugar na kutoka sare dhidi ya Azam FC, kimewashtua mabosi wa Simba na kuamua kuweka kikao kizito kupanga mikakati ya ushindi wakianza na mchezo wa leo watakapoivaa Mtibwa Sugar.
Simba inavaana na Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, unaotarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na uwezo wa timu zote mbili.
Simba ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, wanahitaji pointi nane tu ili kuendelea kulishikilia kombe linalotolewa macho na Yanga waliopo kileleni kwa sasa wakiwa na pointi 83 dhidi ya 82 za Wekundu wa Msimbazi wenye mechi tano mkononi, wakati wenzao wana mbili.
Katika kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mechi zote zilizobaki, vigogo wa Simba juzi na jana walikuwa na vikao kujadili mambo mbalimbali ikiwamo kumaliza ligi kwa kishindo.
Akizungumza na BINGWA jana, Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi, alisema wameipa uzito michezo yao yote iliyobaki ndio sababu ya kufanya vikao mara kwa mara.
Mkwabi aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Simba kwa kishindo mwishoni mwa mwaka jana, alisema watacheza mechi zote zilizobaki kwa nguvu kama walivyofanya kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Mikakati ni kwamba kucheza mechi zote kwa nguvu kama tulivyofanya Ligi ya Mabingwa Afrika na michezo mingine iliyopita, tumejipanga kwa hilo,” alisema Mkwabi.
Kwa upande wake, Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu, alisema wamejizatiti kila idara na fitina zote za ndani na nje ya uwanja ndio sababu waliamua kufanya mazoezi karibu na hoteli waliyoweka kambi.
“Vijana wote wapo fiti hakuna majeruhi, tumejipanga vizuri kuchukua pointi tatu dhidi ya Mtibwa, tumejifua kwenye uwanja ulio karibu na kambi yetu ya Sea Scape, hatujaenda Boko wala Gymkhana,” alisema Rweyemamu.
Naye Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems, alisema siku mbili za mapumziko toka walipocheza na Azam zimetosha kuwarudisha vijana wake mchezoni.
“Ratiba ni ngumu, mechi zipo zimekaribiana lakini tunapambana kuhakikisha tunaibuka na ushindi kwenye kila mchezo tutakaocheza kwa sasa,” alisema.
Msimu huu umekuwa wa kihistoria kwa Simba kutokana na kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa na hata Ligi Kuu Bara, ikibebwa na usajili wa hali ya juu waliofanya, wakinasa wachezaji wa kiwango cha juu na wenye uzoefu kutoka nchi mbalimbali.
0 Comments