BAADA ya kushindwa kulipa kisasi kwa Simba, kikosi cha Azam FC leo kinaingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar.
Azam FC iligawana pointi moja na Simba, Uwanja wa Uhuru na kushindwa kulipa kisasi cha mabao 3-1, waliyofungwa Uwanja wa Taifa mzunguko wa kwanza wa ligi.
Akizungumza na BINGWA, Mratibu wa Azam FC, Philip Alando, alisema wachezaji wote wataanza kuwasili kesho (leo), wakitokea kwenye mapumziko ya muda mfupi waliyopewa.
“Kesho tunaanza maandalizi kwa ajili ya mechi yetu na Mtibwa, baada ya wachezaji kutuliza akili zao kwa siku mbili.
“Mechi na Mtibwa ni ngumu, hivyo tuliona kwa kuwa muda mrefu upo hadi tutakapokutana ni vizuri kuwapa nafasi wachezaji kupumzisha akili pamoja na kufurahi na familia zao na watakaporejea watakuwa na nguvu mpya,” alisema.
Azam FC itakuwa wenyeji mbele ya Mtibwa Sugar katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Chamazi, Mei 22 huku wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa bao 1-0 dimba la Manungu, Turiani.
0 Comments