Windows

Kipigo Jangwani, Simba imehusika

WAKATI nyota wa Yanga wakilia na kipigo walichopewa na Lipuli wakiamini kina mkono wa Simba, huku wakiamini Azam imefurahishwa kutolewa kwao katika michuano ya Kombe la FA, hali ni tofauti kwa kocha wa Chamazi Abdul Mingange aliyekiri wana kazi nzito fainali za FA dhidi ya Wanapuluhengo.
Nyota wa Yanga wanaamini kichapo cha mabao 2-0 walichopewa na Lipuli kwenye mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la FA ilikuwa na mkono wa Simba na Azam ambao ndio wapinzani wao wakubwa kwa madai hawakutaka kuona wafuzu fainali ya michuano hiyo.
Beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ alisema walistaajabishwa na kiwango walichokionyesha Lipuli ndani ya dakika 90 na kudai huenda walifanya hivyo kwa kupata nguvu kutoka kwa watani zao ambao walikuwa wakiombea njaa wapoteze.
“Binafsi nimejisikia vibaya baada ya kukosa tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa kwa mara nyingine tena, hiyo ilikuwa nafasi kubwa kwetu ingawa kwenye ligi bado hatujakata tamaa, lakini bado naamini Simba na Azam wameingiza mkono huku,” alisema Ninja na kufafanua;
“Wachezaji wa Lipuli walipata nguvu kubwa na kucheza kwa mzuka, huku wakichagizwa na shangilia ya mashabiki wa Simba waliojazana Uwanja wa Samora kuwaunga mkono.
Kwangu ni kitu kibaya huu ni msimu wa pili tangu nijiunga Yanga, sijavaa medali yoyote.”
Alisema Azam FC ni kama wachekelea kwa kucheza na Lipuli katika fainali za FA kwani anaamini kama wao wangeingia na kuvaana na Wanalambalamba ushindani ungekuwa mkubwa kwani kuila moja ana hamu ya kuwakilisha nchini.
Naye Deus Kaseke alisema kutolewa kwao kumewaumiza na kudai wapinzani wao walipata nguvu kubwa ya mashabiki wa Simba na mechi ilikuwa ngumu kama wanacheza ya watani wao.
“Tulikuwa tunacheza mechi ngumu kama ya watani wa jadi kwa maana ya Simba na Yanga ndani na nje ya uwanja,” alisema.
MSIKIE KOCHA MINGANGE
Hata hivyo Kocha Mkuu wa Muda wa Azam, Abdul Mingange alitofautiana na mawazo ya nyota wa Yanga kwa kuamini timu yake imepata mchekea.
“Lipuli sio timu ya kubeza mpaka inafika fainali ina maana imeonyesha ushindani huko ilikotoka, hata ukiangalia kwenye ligi si wabaya, Azam tunatakiwa kujipanga vilivyo pengine hata kuliko tungecheza na Yanga,” alisema Mingange na kuongeza;
“Pia imeleta tafsiri kwamba soka halitaki mazoea hivyo klabu za mfano dhidi ya nyingine kwa maana ya Simba, Yanga na Azam FC zinatakiwa kuwa na wachezaji wa kupambana kweli kweli lasivyo kuna kuumbuka.”
Azam ilifuzu fainali hizo mapema baada ya kuifyatua KMC kwa bao 1-0 kabla ua Lipuli kuizima Yanga iliyokuwa ikipiga hesabu ya kukata tiketi ya CAF kupitia michuano hiyo ili msimu ujao icheze Kombe la Shirikisho Afrika kwani njia ya kubeba taji Ligi Kuu ni ngumu.

Post a Comment

0 Comments