IMEELEZWA kuwa klabu ya Yanga ipo kwenye mchakato mkubwa wa kufanyia maboresho kikosi hicho kwa kusajili nyota ambao wataifanya iwe ya kimataifa na yenye ushindani mkubwa kuliko msimu huu ambao kwa sasa upo hatua za lala salama.
Mpaka sasa, Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera amesema kuwa anasubiria fedha tu ili aanze kufanya usajili na ana imani mashabiki wa Yanga watapenda wenyewe na kusahau yote yaliyopita.
Mchakato wa kwanza ni upande wa mbadala wa mlinda mlango namba moja wa sasa Klaus Kindoki, ambapo imeelezwa kwamba mlinda mlango wa Bandari FC, Farouk Shikala anawindwa kusaini msimu ujao.
Harrison Mwenda, anakipiga Kariobangi Sharks ya Kenya aliwapa taabu alipocheza nao kwenye michuano ya Sport Pesa Cup, anacheza nafasi ya kiungo pamoja na Duke Abuya ambaye ni mshambuliaji.
Habari kutoka ndani ya Sharks zimeeleza kwamba wamepata taarifa hizo hivyo wanachosubiri ni utaratibu ufuatwe ndipo wajue hatma ya wachezaji wao hao.
Pia yupo nyota mwingine anayekipa FC Lupopo, Rodrick Mutuma ambaye ni kiraka.
Dili la mshambuliaji wa Gor Mahia ya Kenya, Jacques Tuyisenge ndiye pasua kichwa kwa sasa ndani ya Yanga kwani imeelezwa kuwa dau lake ni moto wa kuotea mbali naye anawindwa pia na AS Vita ambao wapo tayari kutoa milioni 400 ili kuinasa saini ya nyota huyo.
Kwa bongo, winga machachari wa KMC, Hassan Kabunda naye yumo kwenye orodha ya majina hayo ambao imeelezwa wanatakiwa kuvaa uzi wa njano pale Jangwani pamoja na Salum Ilanfaya.
Habari zimeeleza kuwa kupatikana kwa viongozi wapya ambao waliahidi kufanya maboresho makubwa baada ya kuteuliwa kunawapa nguvu ya kufanya usajili waoautaka kwa ajili ya msimu ujao.
Kama mipango itakwenda kama ilivyopangwa inaelezwa kuwa msimu ujao Yanga itafanya makubwa zaidi ya msimu huu ambapo mpaka sasa inaongoza ligi ikwa imejikusanyia jumla ya pointi 80.
0 Comments