Windows

JUMBA LA MENGI LAIBIWA VITO VYA THAMANI


Huku bado familia inaomboleza kifo cha mfanyabiashara tajiri, Reginald Mengi aliyefariki mapema mwezi huu, wapo ambao wamefaidika kiharamu na msiba huo; wameiba vito, vifaa vya thamani na fedha taslimu katika nyumba mbili tofauti.

Vitu hivyo, ambavyo ni mikufu ya dhahabu, kompyuta mpakato pamoja na fedha taslimu ambazo kiwango chake hakijaelezwa, ni mali ya familia na waombolezaji na zilikuwa katika jumba la kifahari la mjane wake, Jacqueline Mengi na katika ya familia ambako mwenyekiti huyo wa kampuni za IPP alizikwa Alhamisi iliyopita.

Mengi, ambaye pia anajihusisha na uchimbaji madini na kumiliki vyombo vya habari, alifariki Mei 2 akiwa Dubai, Falme za Kiarabu alizika kijijini kwao Nkuu, Machame mkoani Kilimanjaro.

Msemaji wa familia hiyo, Benson Mengi alisema kwa sasa hawawezi kuzungumzia jambo hilo kwa kuwa bado uchunguzi unaendelea.

“Bado uchunguzi wa polisi unaendelea,” alisema Benson ambaye ni mtoto wa mdogo wake na Reginald Mengi anayeitwa Benjamin Mengi.

Kamanda wa polisi mkoa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema tayari wanawashikilia watu wawili wakiwatuhumu kuhusika na wizi huo.

Kamanda Issah alisema tukio hilo limefanywa na watu wanaodaiwa kuwa wa ndani na familia hiyo na taarifa zinaonyesha walitokea jijini Dar es Salaam.

“Ni kweli nyumbani kwa Mengi kumeibiwa,” alisema kamanda huyo.

“Suala hilo ni la ndani na tukianza kulishughulikia kikamilifu litahusisha watu ambao ni wa ndani. Sasa sijui tutakuwa kwenye msiba au tutakuwa tunakamatana, maana tumeongeza huzuni juu ya huzuni.

“Kumetokea watu mchanganyiko. Familia ile watu wengi walikuwa haifahamiani, matokeo yake kila mtu anasema mimi na kila mtu anaingia mahali ambako hahusiki na matokeo yake ni wizi.”

Alisema tayari polisi inamshikilia mwanamume na mwanamke mmoja ambao wanaonekana ni wageni wa familia hiyo.

“Ila bado tunaendelea na uchunguzi, ili kubaini undani zaidi wa tukio hili na kuwapata wahusika,” alisema.

Alisema baadhi ya watu ambao hawakutaka majina yao yatajwe, walidai baadhi ya waliohusika walikuwa wamevalia vitambulisho vilivyoandikwa IPP.

Mengi, 77, alikuwa anajihusisha na umiliki wa viwanda kama vya vinywaji baridi, vituo vya televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii, na aliwahi kuongoza taasisi mbalimbali za kibiashara na masuala ya kijamii.

Baada ya kifo cha mfanyabiashara huyo watu wengi walifika nyumbani kwake jijini Dar es Salaam na Machame, Kilimanjaro kwa ajili ya maombolezo.

CHANZO: MWANANCHI

Post a Comment

0 Comments