Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amejibu madai ya rais wa Marekani kuhusu mazungumzo na Iran na kusema: "Donald Trump si mtu wa kuaminika".
Majid Takht-Ravanchi Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameyasema hayo wakati akijibu swali la mtangazaji wa Televisheni ya NBC ya Marekani kuhusu iwapo Iran iko tayari kufanya mazungumzo na Marekani. Takht-Ravanchi aliongeza kuwa: "Awali Rais Donald Trump wa Marekani anapaswa kufafanua ni kwa nini alijiondoa katika meza ya mazugumzo."
Aidha Takht-Ravanchi amesema Trump aliondoka katika meza ya mazungumzo wakati ambao ulimwengu mzima ulikuwa katika meza ya mazungumzo na hata Baraza la Usalama liliidhinisha mazungumzo hayo.
Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, yamkini mazungumzo yakianza, rais wa Marekani kwa mara nyingine atajiondoa katika mazungumzo kwani anapinga na kubatilisha sheria za kimataifa.
Takht-Ravanchi aidha ameashiria madai ya rais wa Marekani kuwa anataka kufanya mazungumzo na Iran kwa lengo la kuizuia kupata silaha za nyuklia
Rais Trump wa Marekani jana aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa: "Nataka viongozi wa Iran wanipigie simu ili tuzungumze kuhusu mapatano mazuri mapatano ambayo yatawasaidia kuondoka katika mgogoro wa kiuchumi."
Trump amedai kuwa, hataki mengi kutoka Iran isipokuwa tu kuhakikisha Iran haimiliki silaha za nyuklia.
Ikumbukwe kuwa mnamo Mei 8 mwaka 2018, Rais Trump wa Marekani aliamua kuondoa nchi yake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, ambayo ni mapatano ya kimataifa, na baada ya hapo akarejesha vikwazo dhidi ya Iran.
0 Comments