Windows

Eti kuishabikia Simba ni zaidi raha!

 Ebwana ehee! Unaambiwa hilo shangwe la mashabiki wa Simba baada ya ushindi mnono walioupata jana Jumatano mbele Coastal Union ni zaidi ya raha.
Simba ilipata ushindi wa mabao 8-1 ambao ni mkubwa kwao tangu msimu huu wa Ligi Kuu Bara uanze.
Mbali na ushindi huo kuwa mnono lakini umenogeshwa na Wekundu hao wa Msimbazi kujikita kileleni mwa Ligi Kuu Bara nafasi ambayo ilikaliwa kwa kipindi kirefu na watani wao wa jadi Yanga.
Mwanachama na mkereketwa wa Simba maarufu kwa jina la Bi Hindu amesema, walichofanya klabu yake ni Zaidi ya raha kwa sababu wamewapa vitu vitamu.
"Simba yeyote anayelala chini kichwa chache anapokinyanyua juu na kutazama wapi nyama inatokea lazima aipate tu. Awe Swala na wengine atamkimbiza na kumrukia shingoni kisha kumnyosha damu na kula nyama,"alisema Bi Hindu.
Amezungumzia nafasi ya ubingwa wa Simba na kusema kwanza anachomwomba ni Mwenyezi Mungu. Pili wachezaji wote washirikiane na kufanya kazi kwa ajili ya Simba, anayepangwa apewe ushirikiano na wote wakipongezana na si kusababisha matatizo,"alisema Bi Hindu.
"Pia, viongozi wangu wawe kitu kimoja, washirikiane na kufanya kazi wasimtafute mchawi lakini pia mfadhili wangu Mohammed Dewji 'Mo Dewji' namwomba Mungu amweke na kumtunza."
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo mashabiki wametamba kwa kusema, ni zaidi ya raha kuwa shabiki wa Simba.
"Ukiwa shabiki wa Simba kwa sasa ni zaidi ya raha unaambiwa. Kila mtu ashinde mechi zake sasa,"alisikika shabiki mmoja wa Simba.
Simba inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 81 baada ya kucheza mechi 31, ikifuatiwa na Yanga wana pointi 80 baada ya kucheza mechi 34 idadi sawa na matajiri wa Azam FC ambao wanashika nafasi ya tatu na pointi 67.
Klabu ambazo zinapambana mkiani mwa Ligi Kuu ni African Lyon iliyo ya mwisho na pointi 22, Mwadui FC ni wa pili kutoka mkiani wakiwa na pointi 37 ambazo ni sawa na za Biashara United iliyo ya tatu huku Alliance FC ikishika nafasi ya nne wakiwa na pointi 38.


Post a Comment

0 Comments