Na Saleh Ally
UONGOZI mpya wa Yanga umeingia na kuanza kazi rasmi ikiwa ni siku moja tu baada ya kuchaguliwa. Bahati mbaya, umeanza kazi mambo yakiwa mabaya.
Yamekuwa mabaya kwa kuwa siku uongozi mpya ulipoanza kazi, ndiyo siku ambayo klabu hiyo ilipoteza nafasi yake ya kushiriki michuano ya kimataifa kwa msimu ujao.
Yanga ilipoteza nafasi hiyo baada ya kufungwa na Lipuli FC katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC). Ilifungwa kwa mabao 2-0, maana yake, haina nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa labda kama itafanikiwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao kimahesabu inaonekana nafasi kubwa iko kwa mabingwa watetezi Simba, labda waboronge wenyewe.
Wakati Yanga ikipoteza mechi yao dhidi ya Lipuli FC, mwenyekiti mpya, Dk Mshindo Msolla na baadhi ya viongozi walioingia madarakani walikuwa kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa na kushuhudia namna mambo yalivyokwenda.
Vizuri wameona na majibu ya mwanzoni yanawaonyesha kwamba kazi haitakuwa laini mbele yao. Wana kazi kubwa hasa ya kufanya kuhakikisha wanaleta mabadiliko ndani ya klabu hiyo kongwe.
Mabadiliko ya Yanga, yatatokana na ushirikiano wa hali ya juu ambao kwa sasa upo kwa kiwango cha kawaida sana. Yanga imepotea njia mara nyingi sana kwa kuwa imekuwa haina uongozi unaotambulika.
Dk Msolla na timu yake, walisema wameshaanza kazi, wakati Yanga inatolewa walishaanza kuitumikia. Binafsi nasema hawapaswi kuingia kwenye lawama badala yake ni nafasi nzuri kwa kuwa wameanza kwa kuyaona machungu ya Wanayanga.
Timu kubwa kama Yanga inapofungwa, wanaoumia ni wengi sana na maumivu yao yamekuwa na mwendelezo wa muda mrefu ukiwemo ule unaobashiri kwamba Yanga ina matatizo makubwa ya kifedha.
Hivyo kinachotakiwa kwa timu ya Dk Msolla ni kuanza kazi mara moja na hakutakiwi kuwa na mipango mingi sana inayosubiri utekelezaji hapo baadaye. Utekelezaji unatakiwa kuanza mapema ili kuikomboa Yanga.
Kwa nini utekelezaji uanze mapema? Jibu ni kwamba Yanga wamekuwa wakiumia mfululizo na huu ni msimu wa pili wanajiona hawana nafasi kama waliyoizoea na bahati mbaya zaidi, Dk Msolla na walioingia naye katika uongozi si mamilionea kama ilivyokuwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji.
Kama Dk Msolla si milionea na wenzake walioingia madarakani nao si mamilionea, wataisaidia vipi Yanga? Maana wanatakiwa kuwa na plani ya muda mfupi na ile ya muda mrefu na zote zinahitaji fedha!
Sote tunakubali, walioshinda kuna mchanganyiko wa wasomi na wale wenye weledi. Tunaamini inawezekana kabisa bila ya kuwa na mwenyekiti milionea na Yanga ikafanya vizuri lakini lazima kuwa na mipango thabiti inayofanyiwa utekelezaji.
Ile mipango ya muda mfupi, ipangwe. Mara moja ianze kufanyiwa utekelezaji ambao lazima uwe wa mipango sahihi utakaoiwezesha Yanga kuingiza fedha kwa matundu sahihi na si kutembeza vikapu vya michango kwenye majukwaa, hili si sahihi.
Mipango iliyozungumzwa kwenye kampeni iingie kwenye karatasi na mara moja utekelezaji uanze. Tukubali kwamba Yanga ina wateja wa mambo mengi ambayo Yanga wanapaswa kuyauza.
Yanga ina jina kubwa ambalo wadhamini wengi watakuwa tayari kuingia na kufanya nayo kazi. Lakini tujiulize, mazingira yanaruhusu? Kuna hali ya kumfanya mtangazaji ajione yuko katika mazingira yatakayoitangaza biashara yake?
Kawaida anayeingiza fedha yake anataka kupata matokeo yanayoisaidia biashara yake. Je, Yanga kuna mazingira hayo na watu watakuwa tayari kutoa fedha zao?
Hii ndio kazi ya Dk Msolla katika plani ya muda mfupi, kwanza kutengeneza mazingira ya kuaminika. Kuanzia kwa wadhamini lakini mashabiki na wanachama ambao badala ya kuchanga kwenye vikapu, wataanza kuichangia Yanga kwa kununua bidhaa zake.
Kuna makampuni mengi yanaweza kuwa tayari kutengeneza bidhaa mbalimbali za Yanga kama maji, jezi, fulana, bendera, soksi, vishika ufunguo na kadhalika vyenye nembo ya Yanga na baada ya hapo wakaingia kwenye mgawo na klabu hiyo.
Kikubwa iwe biashara yenye uwazi, mikataba ya kiufundi inayokubalika na kuaminika na baada ya hapo maisha mapya yaanze.
Yote yanawezekana lakini kwa pamoja tukubali kwamba maisha yaYanga yamo mikononi mwa timu ya Dk Msolla. Wakiweza waiinue na kuanza maisha mapya, wakishindwa waididimize na kuiangamiza.
0 Comments