Katika mazoezi ya mwisho kabla ya mechi yao ya jana dhidi ya Coastal Union, Simba juzi Jumanne ilifanya mazoezi kwenye kiwanja cha ndani kilichopo ndani ya Hoteli ya Sea Scape na nahodha wao, John Bocco aliyekuwa majeruhi tangu aumie katika mechi dhidi ya JKT Tanzania, alirejea uwanjani akipiga tizi pekee yake kabla ya kusimamiwa na kocha.
Bocco alisimamiwa mazoezi yake baadaye na Kocha wa Viungo, Adel Zrane, ikiwa ni habari njema kwa mashabiki wa klabu hiyo waliomkosa nahodha wao kwenye mechi dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons ambazo kote huko mnyama alitakata ugenini.
Mbali na Bocco, pia beki wa kati Salim Mbonde alioyeumia msimu uliopita naye amerejea ingawa hajaanza kufanya mazoezi na wenzake, isipokuwa akijifua kwenye gym ikiwa ni ishara ya kurejea tena uwanjani baada ya kukosekana kwa muda mrefu.
Mbali na majembe hayo, pia Pascal Wawa aliyeumia nyama za paja katika mechi ya kwanza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe naye anajiandaa kurudia uwanjani baada ya kuruhusiwa kuanza kujifua kuanzia Mei 14, siku ambayo timu yake itakuwa ikirudiana na Azam katika mechi ya Ligi Kuu Bara.
Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema kurejea kwa Bocco ni faida kwao kwani wapo katika harakati za mwisho ambazo watatumia nguvu nyingi ili kushinda mechi tano ambazo watacheza hapa Dar es Salaam, kwani wakifanya hivyo watajirahisishia kazi ya kuutetea ubingwa wao.
“Majeruhi wengine kama Wawa mwanzo wa wiki ijayo kwa taarifa za daktari naye ataanza kufanya mazoezi na wenzake, lakini kwa kipindi hiki nitawatumia hawa waliokuwepo kwani hata Adam Salamba ambaye alikuwa na matatizo ya kifamilia ameshayamaliza na amerejea katika timu.”
0 Comments