Windows

Bocco, Aussems wabeba tena tuzo za ubora

John Bocco

NAHODHA wa Simba, John Bocco, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Aprili wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu wa 2018/2019.

 

Bocco ametwaa tuzo hiyo ikiwa ni mara ya pili mfululizo baada ya mwezi Machi kuibuka mshindi wa tuzo hiyo kwa kuwafunika Donald Ngoma wa Azam FC na Jaffari Kibaya wa Mtibwa Sugar alioshindanishwa nao.

 

Bocco ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Emmanuel Okwi wa Simba na Heritier Makambo wa Yanga alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya TPL inayotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

 

Kwa mwezi huo wa Aprili, Simba ilicheza michezo sita na kushinda mitano na kupoteza mmoja, ambapo Bocco alitoa mchango mkubwa kwa timu yake akifunga mabao matatu na kuifanya Simba ipande hadi nafasi ya pili ikitoka ya tatu iliyokuwepo mwezi uliopita.

Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems.

Kamati hiyo pia imemchagua Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems kuwa Kocha Bora wa mwezi Aprili akiwashinda Kocha Mkuu wa Azam, Abdul Mingange na Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera huku mwezi Machi akiwa ametwaa tuzo hiyo.

 

Aussems ameifanya Simba iendelee kung’ara katika ligi hiyo, ambapo kwa mwezi huo ilishinda michezo mitano na kupoteza mmoja ikipanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili.

 

Mingange yeye aliiongoza Azam kushinda michezo mitatu, sare moja na kupoteza mmoja, lakini timu hiyo imeshuka kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili.

 

Kwa upande wa Zahera kwa mwezi huo timu yake ilicheza michezo mitano ikishinda mitatu, sare mmoja na kupoteza mchezo mmoja ikiendelea kubaki kileleni mwa Ligi Kuu Bara. Timu nyingi kwa mwezi huo ukiacha Simba, Yanga na Azam zilicheza mechi chache.

 

Washindi kila mmoja atazawadiwa sh. 1,000,000 (milioni moja) pamoja na kikombe (trophy) kutoka kwa wadhamini Biko Sports, na kisimbusi kutoka Azam Tv ambao ni wana haki ya matangazo ya Ligi Kuu.

MWANDISHI WETU, Dar

ITAKULIZA: Hali ya JACKLINE na MAPACHA Wake, Utawaonea HURUMA!

The post Bocco, Aussems wabeba tena tuzo za ubora appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments