

Kikosi cha Azam kimewasili mkoani Lindi mchana huu na kushangazwa na mapokezi makubwa waliyopata kutoka kwa mashabiki wa soka mkoani Lindi.Azam itacheza fainali wa Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Lipuli Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Ilulu, Lindi.
Katika mapokezi hayo, Azam walipokelewa na mashabiki mbalimbali kwa maandamano kwa mujibu wa kocha wa timu hiyo, meja mstaafu, Abdul Mingange mashabiki hao waliisindikiza timu hiyo hadi hotelini.
"Yalikuwa ni mapokezi ya kushtua, hatukutarajia kitu hiki, mashabiki wetu walikuwa wengi barabarani, wengine kwenye bodaboda ambapo walisindikiza basi la wachezaji hadi hotelini," alisema kocha huyo na kuendelea.
"Mapokezi haya yametuhamasisha na tumejiona tuna deni kwa mashabiki wetu, na malipo yake ni kutwaa ubingwa na kushiriki mashindano ya kimataifa," alisema Mingange.
Akizungumzia maandalizi ya mechi hiyo, kocha Mingange aliyeiongoza Azam kumaliza Ligi katika nafasi ya tatu msimu huu alisema kikosi chake kiko kamili na amekwenda Lindi na nyota wote.
"Nafarijika mpaka sasa sina majeruhi kwenye timu yangu, wachezaji wote wana morali ya ushindi na bila shaka mipango yetu ya kutwaa ubingwa itatimia," alisema.
Azam na Lipuli katika mechi za Ligi Kuu msimu huu zilitoshana nguvu katika mechi zote mbili moja wakitoka suluhu Dar es Salaam na nyingine sare 1-1 mjini Iringa.
Kocha wa Lipuli, Suleiman Matola alisisitiza kutaka kuweka historia ya kuiongoza Lipuli kutwa ubingwa wa FA na kuipeleka kwenye mashindano ya kimataifa.



0 Comments