Windows

Zahera achimba mkwara mzito




USHINDI wa mikwaju ya penalti 4-3 dhidi ya Alliance FC ya hapa uliowapeleka Yanga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam, umempa jeuri Kocha Mkuu wa Wanajangwani hao, Mwinyi Zahera, akiwatunishia msuli wapinzani wao wajao, Lipuli FC.

Baada ya kuiondosha Alliance FC katika hatua ya robo fainali, sasa Yanga watakutana na Lipuli FC ya Iringa katika mchezo wa nusu fainali.


Hata hivyo, Yanga watavaana na Lipuli huku wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Machi 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Samora, mjini Iringa.

Lakini Kocha wa Yanga, Zahera, anaamini kabla ya kusafiri kwenda Iringa, kikosi chake kitakuwa kimejiandaa vya kutosha na kitakuwa imara zaidi kuliko kilivyocheza na Alliance FC.

Akizungumza nasi baada ya mchezo dhidi ya Alliance juzi, Zahera alisema wameivaa Alliance FC wakiwa hawana maandalizi ya kutosha na yeye alikuwa nje ya nchi katika majukumu ya timu ya Taifa ya DR Congo, hivyo wataikabili Lipuli wakiwa wamejiandaa vyema na kushinda mchezo huo ili kutinga fainali na kuzidi kuikaribia ndoto yao ya kutwaa ubingwa huo na kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa.

“Mechi dhidi ya Lipuli lazima tuwe vizuri sana kuliko leo (juzi), kwa sababu tutapata muda wa kujiandaa.

“Leo (juzi) tumecheza kawaida na chini ya kiwango kwa sababu hatujapata maandalizi ya kutosha, hatukupata mchezo wa kirafiki tangu tulipocheza na Lipuli na baadhi ya wachezaji wametoka kwenye timu za taifa,” alisema.

Post a Comment

0 Comments