Windows

Simba yawatafuna KMC, sasa ni masehabu kwa Biashara

Wekundu wa Msimbazi Simba wameendelea kufanya vizuri kwenye bilinge bilinge za Ligi kuu Tanzania Bara baada ya kuifunga KMC kwa goli 2-1 mtanange uliochezwa uwanja wa CCM Kirumba, huku KMC ikiwa nyumbani.

Goli la kwanza la Simba likifungwa na Emmanuel Okwi dakika ya 23 akimalizia pasi ya James Kotei na kuzamisha moja kwa moja mpira kimiani. Bao la Okwi linakuwa la tatu akifunga mfululizo, akiwa amefanya hivyo dhidi ya Kagera Sugar akafunga pia mbele ya Alliance na leo mbele ya KMC na anafikisha jumla ya mabao 10.

Kipindi cha pili KMC walizidisha mashambulizi na kusawazisha dakika ya 57 goli lililopachikwa kiufundi na Hassan Salum Kabunda akitumia makosa ya beki Zana Coulibaly. Kunako dakika ya 75 Mwamuzi Abdallah Kambuzi aliizawadia Simba penalti baada ya mchezaji wa KMC kuunawa ndani ya 18 penalti ambayo ilidakwa na Jonathan Nahimana kwa kumzidi ujanja Kagere.

Mzamiru Yassin aliyeingia kuchukua nafasi ya Kotei akatengeneza penalti nyingine kwa Simba iliyopigwa na nahodha John Bocco dakika ya 82. Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha alama 66 akijikita nafasi ya pili kwa idadi ya mabao ambayo anayo kibindoni tofauti na Azam FC.

Simba wamefunga jumla ya mabao 53 huku Azam FC wakiwa na mabao 49 kibindoni kwa sasa. Baada ya mchezo huo Simba itacheza dhidi ya Biashara United siku ya Jumamosi Uwanja wa Karume, Mara. Kocha Patrick Ausseums amesema watafanya mazoezi siku moja kabla ya mchezo huo licha ya siku moja kutotosha kurekebisha makosa ya mchezo uliopita.


Post a Comment

0 Comments