Windows

Mkuu wa kandanda la Ujerumani Grindel abwaga manyanga

Rais wa Shirikisho la Kandanda la Ujerumani – DFB Reinhard Grindel amejiuzulu baada ya kukiri kuwa alipokea saa ya thamani ya euro 6,000 kama zawadi kutoka kwa aliyekuwa kiongozi wa shirikisho la kandanda la Ukraine.

Hatua hiyo ya kujiuzulu pia inafuatia ripoti za vyomvo vya habari nchini Ujerumani kuhusu malipo aliyopokea kutoka kwa chama mshirika wa DFB. Grindel aliiambia bodi ya DFB kupitia mkutano wa njia ya simu kuwa anajiuzulu maramoja. Taarifa ya shirikisho hilo imemnukuu Grindel akisema kuwa “amesikitishwa sana” kuwa sasa imebidi awachie wadhifa huo wa urais kufuatia kile alichokieleza kuwa ni “ukosefu wangu wa hatua isiyochukuliwa kama mfano mzuri.”

Hadi pale mkuu mpya wa DFB atakapochaguliwa katika mkutano mkuu wa Septemba, makamu wa rais Rainer Roch na Reinhard Rauball watakuwa katika jukumu hilo katika nafasi za ukaimu.

Grindel mwenye umri wa miaka 57, ataendelea kushikilia nyadhifa zake za kimataifa kwenye Baraza la FIFA na kamati kuu ya UEFA, na akasema atairipoti zawadi hiyo ya saa kwa vyama hivyo viwili vya kandanda.

Kabla ya habari za saa kufichuliwa Jumanne, Grindel, ambaye amekuwa rais wa DFB tangu Aprili 2016, alikuwa chini ya shinikizo kuhusu malipo aliyopokea kutoka kwa kitengo ndugu na DFB. Alikanusha usiri wowote kuhusu mapato ya ziada ya euro 78,000 aliyopewa kama mkuu wa bodi ya usimamizi wa kitengo hicho, cha DFB-Medien Verwaltungs-Gesellschaft. Idara hiyo ya habari ya DFB ilisema Grindel alitangaza wazi malipo ya ziada wakati alichukua hatamu za uongozi.


Post a Comment

0 Comments