TAIFA Stars imenoga. Jana jioni kwenye Uwanja wa Taifa kikosi kizima kilipiga tizi la kufa mtu. Mbwana Samatta ambaye ni straika namba moja wa Tanzania akiwa sambamba na wenzie wanaocheza nje kama Simon Msuva, Himid Mao na Thomas Ulimwengu waliongoza mazoezi hayo jambo ambalo lilizidisha hamasha kwa mashabiki na Kocha Emmanuel Amunike.
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Harrison Mwakyembe jana alikitembelea kikosi cha Stars katika mazoezi ya Taifa akiwa sambamba na Mwenyekiti wa BMT, Leodgar Tenga.
Mwakyembe aliambatana pia na mkurugenzi wa Wizara ya Michezo, Usufu Singo na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau ambao walitoa hamasa kwa wachezaji. Stars inaendelea na mazoezi ya kujiandaa dhidi ya Uganda kuwania kufuzu Afcon itakayofanyika nchini Misri mwaka huu.
Waziri alipata dakika 15 kuzungumza na wachezaji kwa kuwataka kupigana kufa na kupona ili kushinda mchezo huo. Akizungumza na Waandishi wa habari Mwakyembe alisema kuwa ; “Wachezaji wanatakiwa kupigana kufa na kupona ili tuweze kufanikisha kushinda mchezo huu, Uganda ni timu ya kawaida tunawaweza kikubwa mashabiki wajitokeze kwa wingi kuja kuishangilia timu yao iweze
kushinda.”
” Kocha Amunike anajiamini sana hata Wachezaji,”alisema Mwakyembe. Lakini Amunike akizungumza na waandishi alisema; “Tunajua tuna mchezo mgumu, hatuhitaji kurilaksi, tunahitaji kuweka rekodi ya Tanzania, tuna kazi ya kuhakikisha tunafuzu mashindano haya.”
” Nimekaa na wachezaji wangu na tayari nimeshawaeleza wanatakiwa wafanye nini na wanajua tunatakiwa tufanye nini Jumapili.
” Tulicheza nao Uganda nyumbani kwao tulipambana na kupata matokeo yale na hakuna aliyeamini hivyo tunahitaji kupambana hapa nyumbani mbele ya kaka, dada, mama na baba zetu ili tuweze kushinda, tunajua wenzetu wameshafanikiwa kufuzu lakini naamini kwa kumtumainia Mungu tutafuzu.
“Nimefurahi kuona wachezaji wote wa kimataifa wapo vizuri na kila mmoja anaonyesha nia ya kutaka kufuzu,” alisema Amunike ambaye ni mchezaji wa zamani wa Barcelona na Nigeria.
0 Comments