KIKOSI cha Simba kimewatambua wapinzani wake katika hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF), mechi ambayo itachezwa Aprili 6, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kabla ya wiki moja kurudiana nao Lubumbashi DR Congo.

Ratiba na droo iliyofanyika kule Misri, jijini Cairo juzi Jumatano, Makao Makuu ya CAF, Simba imepangwa kukipiga na TP Mazembe ambayo katika hatua ya makundi ilimaliza ikiwa kinara wa Kundi C.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema kufanya vizuri kwa timu yao ni kutokana na mambo matatu.

Kwanza ni kuwapa wachezaji wao mahitaji yao kwa wakati kama posho na mishahara ambayo ilikuwa inaongeza ari ya kushindana kwa kila mchezaji ili kupata nafasi ya kucheza na timu kushinda kwasababu walikuwa wanapata zaidi.

Alisema, “Katika hatua hii ya robo fainali tutakuwa tunatoa posho zaidi ya tuliyokuwa tukiitoa hatua za mwanzo pale timu yetu ilipokuwa ikishinda kama tutashinda mechi yoyote dhidi ya Mazembe.

“Kingine mdhamini wetu Mohammed Dewji ‘MO Dewji’ tangu ameanza kuwa nasi, timu ameongeza morali kwa wachezaji na benchi la ufundi hasa akiwa anakutana nao mara kwa mara na kuwaeleza siri ya kufanikiwa katika maisha.

“Si jambo rahisi kupata nafasi ya kuzungumza mara kwa mara na MO Dewji, hilo lilikuwa linawapa msukumo mkubwa wachezaji wetu kuamini kuna kila sababu za kucheza kwa kushindana kufikia malengo.

“Sasa baada ya kufanikisha jambo kubwa la kutinga robo fainali ambayo ni hatau kubwa kabisa katika maisha ya soka la Tanzania malengo yetu mapya ni kucheza fainali jambo ambalo linawezekana,” alisema Try Again ambaye alikuwa Kaimu Rais katika uongozi uliomaliza muda wake.

Try Again, ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba alisema baada ya droo hiyo, wameweka malengo mapya ya kucheza fainali na kuchukua ubingwa wa Afrika kama anavyotaka mwekezaji wao, MO Dewji.

“Kama tuliweka malengo ya awali kufika hatua ya makundi na tukafanikiwa nadhani ilikuwa lazima tuweke malengo mapya ambayo ni kucheza fainali na kuchukua ubingwa huo na kama tukiweza kucheza vizuri mechi zilizobaki inawezekana,” alisema Try Again ambaye aliiwakilisha Simba kule Misri katika upangaji wa ratiba hatua ya makundi.