KOCHA wa timu ya Simba, Patrck Aussems amesema walikuwa tayari kukutana na timu yoyote wala walikuwa hawahofii droo ya robo fainali jana na wameshagundua cha kufanya kwenye mechi za ugenini.
Akizungumza nasi Aussems alisema kuwa Simba kwa sasa ni timu kubwa haipaswi kuhofia timu yoyote Afrika hususani kwenye robo fainali.
“Mpira una matokeo ya ajabu hasa kutokana na namna inavyokuwa baada ya dakikia tisini, nina imani na kikosi changu tutapata matokeo kwa timu yoyote.
“Ushindani ni mkubwa kwa kuwa hatua hii ni ngumu na kila timu ni bora, hesabu zetu ni kuona tunashinda katika michezo yetu na kufanyia kazi makosa ambayo tuliyafanya kwenye michezo yetu ya nyuma,” alisema Aussems.
Lakini Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori ambaye jana usiku alishuhudia droo ya robo fainali nchini Misri, alisema;
“Hatua nzuri kwetu na mashabiki kiujumla, baada ya kutimiza lengo la kwanza kwetu kutinga hatua ya makundi, tukabadili mbinu tukapigia hesabu hatua ya robo fainali sasa tunapeleka akili zetu mbali kwenye fainali ya mashindano haya.
“Uwezo tunao tumegundua tatizo kubwa kwetu awali ilikuwa tukitoka nje sasa hilo ndilo tunaloanza kulifanyia kazi kwa sababu nyumbani hatuna cha kupoteza kutokana na rekodi zetu zilivyo pia uwepo wa mashabiki unatufanya tuendeleze rekodi zetu.
“Kikubwa ambacho kinatufanya tuamini kwamba tutatinga hatua hiyo ni mwendo wetu kuwa mdogomdogo lakini wenye malengo makubwa, ipo wazi tulipokea vichapo vibaya sana ugenini ila vimetukomaza, pia fedha kwetu ipo hatuna tatizo,” alisema Magori ambaye ndiye kiongozi msomi zaidi kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.
Simba walitinga hatua hiyo kwa kuwaondosha Wakongo AS Vita Club kwa mabao 2-1 katika Uwanja wa Taifa, wiki iliyopita.