Simba SC inashuka uwanjani kumenyana na Ruvu Shooting ya Pwani katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaofanyika Uwanja wa Taifa Jijini DSM kuanzia majira ya saa moja jioni, Jumanne ya Machi 19.
Wanamsimbazi wanashuka kwenye mchezo huo ikiwa ni siku tatu toka wametoka kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita ambapo iliibuka na ushindi wa goli 2-1.
Kuelekea mtanange huo Msemaji wa Ruvu Shooting Masau Bwire amesema “Lolote linaweza kutokea, timu imejiandaa vizuri kupata alama tatu, hivyo mashabiki wa mpira wasije na matokeo yao mfukoni jambo ambalo litakuwa na athari kubwa kutokana na matokeo yanayoweza kujiri uwanjani” Alisema Bwire ambaye mbali na usemaji wa klabu, ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Makumbusho.
Wakati huo huo Simba kupitia kwa Patrick Ruyemamu ambaye ni Meneja wa timu hiyo amesema timu iko katika hali nzuri baada ya kupata matokeo mazuri kwenye Ligi ya Mabingwa jambo ambalo linawapa hamasa wao (Simba).
Simba ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa TPL ikiwa na alama 51 katika michezo 20 ambayo imecheza wakati Ruvu Shooting inakamata nafasi ya 17 Sawa na mitanange 30 alama 35.
Ili kujiweka katika mazingira mazuri zaidi Shooting inahitaji kushinda mchezo huo ambapo utaiongezea pointi na kujitoa katika mstari wa kushuka daraja.
Mchezo wa mwisho Simba iliibuka na ushindi wa goli 3 dhidi ya Stand United ugenini wakati Ruvu Shooting ikiwa inasuasua kwenye mwendelezo wa TPL.
0 Comments