

Droo ya robo fainali Ligi ya Vilabu bingwa Ulaya imeshafanywa huku Ajax Amsterdam waliowabandua mabingwa watetezi Real Madrid wakipangwa kucheza na Juventus ambapo Ajax watakuwa nyumbani katika mechi ya mkumbo wa kwanza.
Liverpool ambao walifuzu kwenye fainali iliyopita ila wakalazwa na Madrid sasa watapambana na FC Porto, mechi ya kwanza ikiwa uwanjani Anfield kisha mechi ya ungwe ya pili ikachezwe Estadio do Dragao nchini Ureno.
Manchester City ambao walikuwa na kazi rahisi katika mechi ya raundi ya timu kumi na sita bora watakuwa na kibarua dhidi ya timu nyengine kutoka Uingereza Tottenham Hotspur kisha Manchester United baada ya kuwaondoa Paris Saint Germain sasa wana mlima mwengine wa kupanda watakapokwaana na Barcelona katika robo fainali, huku mechi ya kwanza ikichezwa Old Trafford na ya marudiano igaragazwe Camp Nou.
Mechi za kwanza za robo fainali zitachezwa Aprili 9 na 10 huku mechi za marudiano zikichezwa Aprili 16 na 17. Michuano ya nusu fainali itakuwa Aprili 30 na Mei 1 halafu mechi za marudiano zichezwe Mei 7 na 8.
Fainali ya mwaka huu itakuwa Madrid katika uwanja wa nyumbani wa Atletico Madrid, Wanda Metropolitano.



0 Comments