KAMA Taifa Stars wakiipiga Uganda Jumapili jijini Dar es Salaam, kila mchezaji ana uhakika wa Sh. Mil 11 na ushee ambazo kwa Dar es Salaam unapata kiwanja na chenji inabaki. Hiyo inaami nisha kwamba Shiza Kichuya mwenye viwanja kadhaa Morogoro, kama Stars ikishinda Jumapili ana uwezo na akahamia kabisa.
Kamati maalum ya Saidia Stars imeweka wazi kwamba vijana watafurahia maisha kama wakilipa Taifa heshima ya kufuzu Afcon itakayopigwa baadae mwaka huu nchini Misri.
Uganda wao wameshafuzu na jana kwenye mitandao yao ya kijamii walikuwa wanatamba kwamba wapo kambini Misri kuzoea hali ya hewa tayari kwa fainali, wala Stars haiwaumizi kichwa.
Kamati hiyo inaogozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pamoja na Mkandarasi Hersi Said ambaye ni Katibu, ina wajumbe wazito 12.
Kwa mujibu wa gazeti la Spoti Xtra linaloaminika zaidi kwa takwimu za michezo kila Alhamisi na Jumapili, Hersi alisema wameona ni vyema kutoa motisha ya zaidi ya Dola 5,000 (zaidi ya Sh.11 milioni) kwa kila mchezaji ili kuonyesha thamani na umuhimu wa mchezo huo.
“Tutawapa kila mchezaji zaidi ya Dola 5,000 endapo tutafuzu kwa kuifunga Uganda, pesa hizi ni kama kuwapa morali vijana wetu ili tuhakikishe tunaibuka na ushindi na hii ndio kazi ya kamati yetu kuhakikisha tunafanya kila njia kuhakikisha timu ya taifa inafanikiwa,” alisema na kuongeza.
“Tunawaomba sana mashabiki wajitokeze kwa wingi kuishabikia timu ya taifa hasa wanapofika uwanjani wanatakiwa kushangilia kwa nguvu,kama mashabiki wakijitokeza kwa wingi basi tutapata ushindi kwa kuwa mashabiki ndiyo kila kitu.”
Hersi licha ya kusema hivyo, lakini Spoti Xtra linafahamu zawadi hiyo inaweza kuongezeka na kutamkwa lolote wikiendi hii.
Kama Stars itafuzu itakuwa neema kwa Tanzania, kwani tayari Simba imefuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na inazidi kupepea kwenye rekodi za ubora.
0 Comments