Kuondolewa kwa Paris Saint Germain katika Champions League kumeiacha klabu hiyo ikiwa na mshtuko mkubwa na ikitafuta majibu lakini hakutakuwa na hatua ya haraka ya kumtimua kocha Thomas Tuchel baada ya Wafaransa hao kuanguka mtihani kwa mara nyingine tena katika jukwaa la Ulaya. Hayo ni kwa mujibu wa rais wa PSG Nasser Al-Khelaifi.
Mabingwa hao wa Ufaransa walitupa faida ya mabao 2 – 0 waliyokuwa nayo kutokana na mechi ya mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 dhidi ya Manchester United mjini Paris Jumatano usiku, na kuondoka kwa kanuni ya mabao ya ugenini baada ya kuzabwa 3 – 1 katika dimba la Parc des Princes.
PSG wametumia kiasi kikubwa cha hela wakikusanya kikosi chenye uwezo wa kushinda kinyang’anyiro hicho maarufu Ulaya, lakini wameshindwa kupenya Zaidi ya hatua ya robo fainali tangu iliponunuliwa na kampuni ya Uwekezaji Wa Michezo nchini Qatar mwaka wa 2011.
“Nimesikitishwa sana na matokeo na mchezo huo. Sielewi ni kwa nini tulishindwa,” Alisema Al Khelaifi.
PSG ilimteuwa Tuchel mwezi Mei katika matumaini kuwa Mjerumani huyo jasiri angefanikisha ndoto yao ya kupata mafanikio katika Ligi ya Ulaya, na Khelaifi amesema klabu hiyo haitafanya maamuzi yoyote kuhusiana na mustakabali wake katika joto lililopo kwa sasa.
“Nnamuamini kocha…lakini sio kwamba tulishilindwa mechi kwa hiyo tuchukue hatua sasa,” rais huyo alinukuliwa na gazeti la michezo la Ufaransa L’Equipe.
Penalti tata katika dakika za mwisho dhidi ya Presnel Kimpembe kuunawa mpira baada ya refarii kushauriana na mwamuzi msaidizi wa video ilitiwa kimiani na Marcus Rashford. Mabao mawili ya kipindi cha kwanza Romelu Lukaku yaliwabumburusha mabingwa hao wa Ufaransa. Bao la PSG lilifungwa na Juan Bernat.
0 Comments