Windows

HIVI NDIVYO SIMBA ILIVYOWAZIDI WAKONGO KWA KILA KITU TAIFA, PASI 439 ZAPIGWA


ACHANA na mziki wa Simba. Fanya unachofanya lakini ndani ya Uwanja wa Taifa hutoki. Alikuja JS Sauora akapigwa, akasingizia waandishi na magazeti ya Bongo eti ndio yaliwatoa mchezoni. Akaja Al Ahly kwa mbwembwe zote na kikosi chake cha mabilioni. Akakaa Taifa tena kweupe kabisa.

Ijumaa wakatua jamaa fulani wa DR Congo wanaitwa AS Vita.Tena wakakodisha na Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera. Juzi usiku wakala mbili saafi kabisa Taifa, wakawaacha Wakongo wanashangaana. Hiyo ndiyo Simba ya Tanzania ambayo sasa imetinga kwa kishindo hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hakuna cha masebene ya Wakongo wala Ndombolo. Ndio maneno ya mashabiki wa Simba waliyokuwa wakiyatumiakuwakejeli wenzao wa Yanga ambao jana walikuwa wakiisapoti AS Vita.

AS Vita walipata bao la kuongoza dakika ya 13 likifungwa na Kazadi Kasengu huku Mohammed Hussein Tshabalala akisawazisha dakika ya 36 baada ya mabeki na kipa AS Vita kuvurugana na kujikuta wakilamba nyasi. Bao la ushindi lilipatikana dakika ya 90 kupitia kwa fundi Claytous Chama.

Sikia sasa lilivyofungwa, John Bocco alitoa pasi kwa Haruna Niyonzima akausogelea kama anataka kuugusa lakini akaupotezea. Chama akazamisha kitu nyavuni kiulainii kabisa.

Lilikuwa ni shuti la juu. Chama ndiye mchezaji aliyeipeleka Simba hatuaya makundi ya Ligi ya Mabingwa na jana ndiye yeye aliyewakita robo fainali. Simba walikosa nafasi sita za mabaokipindi cha pili kilipoanza, Meddie Kagere na Bocco walikosa mabao ya wazi kwa kushindwa kuunga vizuri pasi za mwisho walizopewa.

Simba walifanya mabadiliko kwa Emmanuel Okwi, Mzamiru Yasin na James Kotei wakaingia Hassan Dilunga, Rashid Juma na Niyonzima Niyonzima alionekana kutawala sehemu kubwa ya mchezo na kucheza atakavyo kitendo ambacho kiliibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii nchini Rwanda na wakashinikiza arudishwe timu ya Taifa.

Makusu Mundele ambaye ni straika tegemeo wa AS Vita anayewindwa na Simba, alipiga shuti moja lililopaa na krosi moja iliyodakwa hadi anatolewa dakika ya 63 katika mchezo huo ambao Simba ilimiliki mpira kwa 53 dhidi ya 47.

Kagere kaotea mara mbili katika kipindi cha pili cha mchezo huo ulioamsha mizuka ya mashabiki wengi. Simba inasubiri ratiba ya robo fainali itakayopangwa wiki hii, ambapo itavaana na timu za Arabuni au TP Mazembe.

Post a Comment

0 Comments